Dar es Salaam. Makamu wa Rais Dk Emmanuel Nchimbi amesema kitendo cha baadhi ya viongozi wa Serikali, taasisi za kijamii, vyama vya siasa na wanaharakati kuendelea kuzungumzia yaliyotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025, nje ya mfumo wa kisheria uliowekwa juu ya jambo hilo, ni kutotendea haki taifa.
Dk Nchimbi amesema hayo leo Februari 2, 2026, alipozungumza wakati wa hafla ya maadhimisho ya Siku ya Sheria na kuanza kwa mwaka wa Mahakama 2026 jijini Dodoma, akiwa mgeni rasmi.
Makamu huyo wa Rais ametoa kauli hiyo akijibu ombi lililotolewa na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, aliyesema TLS inatambua yaliyojitokeza kabla, wakati na baada ya uchaguzi, na kwamba wanapendekeza kila anayehitajika kuwajibika awajibike kwa maslahi mapana ya Taifa.
Baadhi ya washiriki wakiwa katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini 2026, yanayofanyika leo Jumatatu, Februari 2, 2026 jijini Dodoma.
“Katika kipindi hiki, tuwaombe hata viongozi wetu wenye dhamana, anapokuwa hana jambo muhimu sana la kuzungumza, asizungumze jambo ambalo litatonesha mioyo ya wananchi. Tuombe hekima kwa Mungu ili kulirejesha Taifa pamoja.
“Hapa tulipo siko, na tusipokuwa makini huko tutakokwenda siko kabisa, tutafika mahali tutashindwa kurudi tulikotoka. Rai yetu ni kwamba tuangalie namna bora na shirikishi, yenye kuaminika na wote, na msingi wa kutuongoza katika hili iwe ukweli, haki, uwazi na uwajibikaji,” amesema.
Wakili Mwabukusi amesema ni muhimu kama Taifa tuongee kwa ukweli, bila kufarijiana kwamba tumejitia aibu, lakini lazima itafutwe namna ya kutoka na njia hiyo iongozwe na ukweli, haki, uwazi na uwajibikaji.
Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi akizungumza leo Jumatatu, Februari 2, 2026, katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini 2026, yanayofanyika jijini Dodoma.
Akijibu kauli hiyo, Dk Nchimbi amesema: “Nimshukuru Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, Boniface Mwabukusi, ametuasa. Sio vizuri kuzungumzia yaliyojiri Oktoba 29, 2025, kwa sababu yanatonesha kidonda na yanaweza yasisaidie kwenye mchakato wa haki.
“Kwanza, niseme nakubaliana naye kwa asilimia 100; pili, naongezea pale aliposahau, sio viongozi wa Serikali peke yake bali pia viongozi wa vyama vya siasa, taasisi za kijamii na wanaharakati,” amesema.
Dk Nchimbi amesema Rais Samia ameunda tume ya kufanya uchunguzi na inaendelea kufanya kazi, hivyo kuendelea kuzungumzia jambo hilo na wa viongozi wa Serikali, taasisi za kijamii na vyama vya siasa nje ya mfumo wa kisheria uliowekwa ni kutotendea haki taifa letu.
Amesema kila mtu anayeipenda Tanzania ni muhimu akubaliane na Rais wa TLS kwamba watu wasitoneshane, bali vyombo vya kisheria vipewe nafasi kutimiza wajibu wao.
