
Mali imetangaza kulipiza kwa kuweka masharti ya viza kwa raia wa Marekani na kwamba watatakiwa kulipa kiasi cha dola 5,000 mpaka 10,000 kwa viza za Biashara na Utalii kwa raia wanaotafuta vibali vya kuingia nchini humo.
Wizara ya Mambo ya nje ya Mali yenye makao yake Bamako imefikia uamuzi huo jana Jumapili Oktoba 12, baada ya Marekani kutangaza tozo hizo mpya kwa nchi za Afrika ikiwa na lengo la kutaka kulinda mipaka yake na usalama wake, pia Mali imelaani vitendo hivyo ikisema kuwa nchi hiyo inakiuka mkataba wa makubaliano uliosainiwa mwaka 2005.
Taarifa iliyotolewa na Wizara hiyo imesisitiza kuwa Mali imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Marekani katika kudhibiti uhamiaji usio halali kwa kuzingatia sheria na kuheshimu utu wa binadamu, mzozo huu unaibua mvutano mpya kati ya Bamako na Washington.
Mali ni moja ya nchi saba za Afrika zilizoingizwa katika mpango wa majaribio wa mwaka mmoja unaolenga Mataifa yenye kiwango kikubwa cha watu wanaokaa zaidi ya muda wa viza zao, Nchi nyingine zilizoorodheshwa ni Mauritania, Sao Tome na Principe, Tanzania, Gambia, Malawi na Zambia.

