
Klabu ya Manchester United imemfuta kazi Meneja Ruben Amorim kama kocha mkuu klabuni hapo kufuatia msururu wa matokeo yasiyoridhisha ikiwa ni miezi 14 tangu achukue mikoba ya kuinoa klabu hiyo
Taarifa rasmi iliyotolewa na Mashetani hao Wekundu muda mfupi uliopita imeeleza kuwa iungo wa zamani wa klabu hiyo, Darren Fletcher ambaye alikuwa mkurugenzi wa ufundi ameteuliwa kuwa kocha wa muda akitarajiwa kuiongoza timu hiyo dhidi ya Burnley siku ya Jumatano.
“Wakati Manchester United ikishika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, uongozi wa klabu hiyo umefanya uamuzi huo ‘kishingo upande’ ikiona ni wakati muafaka wa kufanya mabadiliko. Hii itaipa timu fursa bora zaidi ya kumaliza juu zaidi kwenye msimamo wa Ligi.” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Uamuzi huo umekuja baada ya kuripotiwa kuongezeka kwa mvutano kati ya bodi ya Manchester United na Ruben Amorim kuhusu fungu la usajili, huku uhusiano kati ya mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo, Jason Wilcox na Amorim ukitajwa kudorora.
