Marekani, Iran kuamua amani au vita Geneva

Rais wa Marekani Donald Trump na Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatolla Ali Khemeni
Mvutano kati ya Marekani na Iran, umefikia hatua nyeti, huku pande hizo mbili zikikutana mjini Geneva kwa mazungumzo mapya kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran.

IHali ya taharuki imetanda Iran na Ukanda wa Mashariki ya Kati, kabla ya mkutano huo.

Marekani na Iran zinafanya duru mpya ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja mjini Geneva, Uswisi, leo.

Lengo ni kumaliza mzozo wa muda mrefu kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran.

Mazungumzo haya yanafanyika katika mazingira ya mvutano mkali wa kijeshi na kisiasa.

Rais wa Marekani, Donald Trump, ameonya kuwa hataruhusu Iran kumiliki silaha za nyuklia. Katika hotuba yake ya hivi karibuni, aliishutumu Tehran kwa kufukuzia malengo hatari ya nyuklia.

Aidha, alidai kuwa Iran inaendeleza makombora yanayoweza kufikia masafa marefu.

Iran imekanusha madai hayo na kusisitiza kuwa mpango wake ni wa amani. Kwa mujibu wa taarifa rasmi, masafa ya makombora yake ni kati ya kilomita 2,000 hadi 3,000.

Hilo ni chini ya umbali wa kufikia bara la Amerika.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema mpango wa makombora wa Iran ni tishio lisilovumilika.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa diplomasia bado ni chaguo. Amesema rais Trump anapendelea suluhisho la mazungumzo kuliko hatua za kijeshi.

Kwa upande wa Iran, Waziri wa Mambo ya Nje, Abbas Araghchi, amesema nchi yake iko tayari kujibu maswali.

Lakini amesisitiza kuwa hawako tayari kuacha haki yao ya teknolojia ya nyuklia kwa matumizi ya amani na kwamba makubaliano ya haki yanawezekana.

Mazungumzo haya yanakuja baada ya maandalizi makubwa ya kijeshi ya Marekani katika Mashariki ya Kati, yaliyoshuhudiwa wiki chache zilizopita.

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema ana mtazamo chanya kuhusu mazungumzo; akitahadharisha kwamba huenda yakamalizika katika hali ya “si vita wala si amani.”

Wachambuzi wa masuala ya Mashariki ya Kati wanasema matarajio ya vita bado yapo. Baadhi wanaamini kuwa safari hii mzozo unaweza kuwa mkubwa zaidi. Hofu hiyo inachangiwa na ongezeko la silaha na vikosi katika eneo.

Hata hivyo, kuna dalili kwamba pande zote zinatambua gharama ya vita. Marekani inasisitiza kuwa diplomasia haijaondolewa mezani. Iran nayo inasema makubaliano yanawezekana ikiwa yatakuwa ya haki.

Mazungumzo ya Geneva yanachukuliwa kama hatua muhimu ya kihistoria. Yanaweza kufungua ukurasa mpya wa maelewano au kuisukuma kanda hiyo kwenye mzozo hatari zaidi. Dunia sasa inasubiri kuona ni njia ipi itachaguliwa.

Chanzo: DW

Related Posts