Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza kuwa Marekani imefanya mashambulizi makubwa ya kijeshi dhidi ya Venezuela na kufanikiwa kumkamata Rais wa nchi hiyo, Nicolás Maduro, pamoja na mke wake.
Kupitia taarifa aliyotoa kwenye mtandao wake wa Truth Social, Trump amesema operesheni hiyo ilifanywa kwa kushirikiana na vyombo vya usalama vya Marekani, huku akieleza kuwa maelezo zaidi yatatolewa katika mkutano na waandishi wa habari uliopangwa kufanyika saa 11:00 asubuhi kwa saa za Marekani Mashariki, katika makazi yake ya Mar-a-Lago, Florida.
Hata hivyo, Rais Trump hakutoa maelezo ya kina kuhusu jinsi Maduro alivyokamatwa wala amepelekwa wapi, wakati serikali ya Venezuela bado haijathibitisha rasmi taarifa hizo.
Awali, Serikali ya Venezuela ilitangaza kuwa inakataa na kulaani kile ilichokiita uvamizi wa kijeshi wa Marekani, ikitangaza pia hali ya dharura ya kitaifa kufuatia mashambulizi hayo.
Mashuhuda waliopo katika mji mkuu wa Caracas wameripoti kusikika kwa milipuko mikubwa, huku video zinazosambaa zikionesha moshi mzito ukifuka na moto ukiwaka katika baadhi ya maeneo.
Kwa muda mrefu, Marekani imekuwa ikiishutumu Nicolás Maduro kwa kuongoza mtandao wa kimataifa wa biashara ya dawa za kulevya, madai ambayo amekuwa akiyakana mara kwa mara.
Marekani pia ilikuwa imetoa zawadi ya dola Milioni 50 kwa mtu yeyote ambaye angeweza kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwake.
Wachambuzi wa siasa za kimataifa wanasema tukio hilo linakuja baada ya wiki kadhaa za mvutano mkubwa, ambapo Rais Trump alikuwa ameongeza shinikizo dhidi ya serikali ya Maduro, sambamba na kuimarishwa kwa uwepo wa kijeshi wa Marekani katika ukanda wa Amerika ya Kusini.
Imeelezwa, taarifa zaidi kuhusu tukio hili zitafahamika baada ya mkutano wa waandishi wa habari uliotangazwa na Rais Trump.
