
Wizara ya Ulinzi ya Marekani imetangaza majina ya Wanajeshi 6 wa Marekani waliouawa Nchini Kuwait Jumapili baada ya ndege ya Iran isiyo na rubani (drone) kushambulia Kituo chao cha kazi katika Bandari ya Shuaiba ikiwa ni siku moja tu baada ya Marekani na Israel kuanzisha mashambulizi dhidi ya Iran.
Hadi Jumanne, Jeshi la Marekani lilisema Wanajeshi sita wa Marekani wamefariki wakiwa kwenye oparesheni dhidi ya Iran Nje ya Nchi ambapo vifo vitatu vilitangazwa Jumapili na vingine vitatu vilitangazwa Jumatatu ambapo Wanajeshi wengine watano wamejeruhiwa vibaya.
“Ni huzuni kubwa na majonzi, tunawatambua na kuwaheshimu Wanajeshi wetu waliotoa sadaka ya mwisho kwa ajili ya Nchi yao, walihudumu bila kuchoka kwa uthabiti na bila woga, walikuwa Mabalozi wa kweli wa uhuru, wanawakilisha ubora wa kile Taifa letu linasimamia, tunaomba Mungu azipe familia zao amani na faraja katika kumbukumbu zao, kamwe hatutowasahau” -Brigedia Jenerali Clint A. Barnes, Naibu Kamanda Mkuu Kituo cha Amri cha Operesheni
