Mawaziri Waitembelea Timu ya Taifa Stars Misri Ikijiandaa na AFCON

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, wameitembelea timu ya Taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, inayojifua kambini jijini Cairo, Misri.

Katika ziara hiyo, mawaziri hao wameikabidhi timu hiyo bendera ya Taifa ikiwa ni ishara ya kuwatakia heri na kuwapa motisha kuelekea kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), itakayoanza hivi karibuni nchini Morocco.

Akizungumza na wachezaji pamoja na viongozi wa timu hiyo, Profesa Kabudi amekiahidi kikosi cha Taifa Stars ushirikiano wa Serikali kwa kiwango cha juu, akisisitiza kuwa serikali itaendelea kutoa msaada unaohitajika ili kuhakikisha timu inafanya vizuri katika michuano hiyo mikubwa na yenye heshima kubwa barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Aidha, Profesa Kabudi amewahimiza Watanzania kuipenda na kuiunga mkono timu yao ya Taifa kwa hali na mali, akiwataka kuishangilia popote itakapocheza, hususan kwa wale watakaopata fursa ya kufuatilia mechi zake moja kwa moja nchini Morocco.

Kwa upande wake, Waziri Kombo amewasihi wachezaji hao, ambao ni wachache kati ya mamilioni ya Watanzania, kutanguliza uzalendo kwanza kwa kuipigania bendera ya Taifa kwa moyo, jasho na kujituma, ili kuliletea heshima Taifa la Tanzania.

Katika michuano hiyo ya AFCON, Taifa Stars imepangwa katika Kundi C pamoja na timu za Nigeria, Tunisia na wenyeji Morocco.

Related Posts