Mgombea wa Urais Uganda Bob Wine Akamatwa na Kuchukuliwa na Helkopta ya Kejeshi

Chama cha National Unity Platform (NUP) kimedai kuwa mgombea urais wa upinzani nchini Uganda, Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, ameondolewa kwa nguvu nyumbani kwake na kuchukuliwa na helikopta ya kijeshi kuelekea kusikojulikana.

Taarifa hiyo iliyotolewa kupitia mitandao ya kijamii jana Ijumaa, imekuja siku moja tu baada ya Waganda kupiga kura katika uchaguzi uliogubikwa na hali ya taharuki na kukatwa kwa huduma za intaneti nchi nzima.

Hadi sasa, serikali ya Uganda haijatoa tamko rasmi kuhusu madai hayo. Maofisa wa NUP wamekiambia kituo cha habari cha Al Jazeera kuwa watu waliovalia sare za kijeshi na usalama waliruka ukuta wa nyumba ya Bobi Wine, ingawa kwa sasa ni vigumu kuthibitisha eneo alilopelekwa kutokana na changamoto ya mawasiliano nchini humo.

Kabla ya tukio hilo, Bobi Wine alikuwa ameweka ujumbe mtandaoni akidai kuwepo kwa “ujazaji mkubwa wa masanduku ya kura” kote nchini na kuwataka Waganda kuukataa kile alichokiita “utawala wa kihalifu.”

Wakati hayo yakitokea, matokeo ya awali yaliyotolewa na Tume ya Uchaguzi Ijumaa jioni yalionesha Rais Yoweri Museveni (81) akiongoza kwa 73.7% dhidi ya 22.7% za Bobi Wine, huku kura 81% zikiwa zimeshahesabiwa. Matokeo ya mwisho yanatarajiwa kutangazwa leo Jumamosi majira ya saa 10:00 jioni kwa saa za Kampala.

Licha ya upigaji kura wa Alhamisi kumalizika kwa amani katika maeneo mengi, machafuko makubwa yameripotiwa usiku wa kuamkia Ijumaa katika mji wa Butambala, takriban kilomita 55 kutoka Kampala.

Jeshi la Polisi limesema watu saba wameuawa baada ya “wahuni” wenye mapanga kuvamia kituo cha polisi, wakati Mbunge wa upinzani, Muwanga Kivumbi, akidai kuwa watu 10 wameuawa baada ya vikosi vya usalama kushambulia wafuasi wa upinzani waliokuwa wakisubiri matokeo nyumbani kwake.

Related Posts