
Mshahara wa Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino, umeongezeka kwa kiwango kikubwa katika kipindi cha uongozi wake, ukifikia Dola za Kimarekani Milioni 6.1 kwa mwaka, sawa na takriban Shilingi bilioni 15 za Tanzania.
Taarifa hiyo imebainishwa kupitia utafiti uliofanywa na Gazeti la Le Monde, unaofichua mwenendo wa malipo ya Rais wa FIFA tangu Gianni Infantino alipoingia madarakani mwaka 2016.
Infantino, raia wa Italia, alichaguliwa kuwa Rais wa FIFA Februari 26, 2016, akichukua nafasi ya Sepp Blatter, aliyelazimika kuondoka madarakani kufuatia tuhuma nzito za rushwa zilizoikumba FIFA na kuitikisa dunia ya soka.
Wakati wa uongozi wa Blatter, mshahara wa Rais wa FIFA ulikuwa Dola Milioni 1.4 kwa mwaka, sawa na takriban Shilingi bilioni 3.5 za Kitanzania. Hata hivyo, tangu Infantino achukue uongozi, kumekuwa na mabadiliko makubwa ya kiutawala, kibiashara na kimkakati yaliyopelekea kuongezeka kwa mapato ya FIFA, jambo lililoambatana na ongezeko la mshahara pamoja na bonasi za Rais huyo.
Ripoti ya Le Monde inaeleza kuwa ongezeko hilo la mshahara limekuwa likifanyika hatua kwa hatua kila mwaka, likionyesha mabadiliko ya mfumo wa malipo ndani ya FIFA, pamoja na msisitizo mkubwa wa ukuaji wa mapato, mikataba ya kibiashara na haki za matangazo ya mashindano ya kimataifa.
Katika kipindi cha karibu miaka 10 ya uongozi wake, Gianni Infantino amejijengea utajiri mkubwa na kutajwa kuwa miongoni mwa viongozi wenye kipato kikubwa zaidi katika mashirika ya michezo duniani. Hata hivyo, suala la mshahara wake limeendelea kuibua mjadala miongoni mwa wadau wa soka, baadhi wakiona ni matokeo ya mafanikio ya kiutendaji, huku wengine wakipinga kiwango hicho wakidai kinapingana na misingi ya uwazi na maadili ya uongozi.
