Miaka 7 Jela kwa Kutumia Vyeti FEKI vya Marehemu


TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkani Kigoma imemkamata na kumfikisha tena mahakamani Neema Moshi aliyekuwa ametoroka baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka saba jela kwa makosa ya kutumia vyeti vya mtu mwingine.

Akizungumza na waandishi wa habari, mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kigoma, Asha Kwariko, amesema mtuhumiwa huyo alitoroka baada ya kuhukumiwa na mahakama Desemba 16, 2024, na kutokomea kusikojulikana kwa takribani miezi 14 kabla ya kukamatwa tena na kufikishwa mahakamani Machi 6, 2026, ili kusomewa hukumu yake.

Kwariko amesema Neema alifikishwa mahakamani kwa makosa manne, ikiwamo kutumia vyeti vya kidato cha nne vya mdogo wake aitwaye Grace Moshi, aliyefariki dunia Januari 4, 2018 akisema baada ya kupokea taarifa, walifanya uchunguzi wa kina na kubaini ukweli wa tuhuma hizo kabla ya kumfikisha mahakamani.

Ameeleza kuwa mtuhumiwa alikutwa na hatia ya makosa ya kujifanya mtu mwingine kinyume na kifungu cha 369(1)(a) na 35 cha Sheria ya kanuni ya adhabu.

Pia alikabiliwa na makosa mawili ya kujifanya mtu mwingine aliyeandikwa kwenye cheti kinyume na vifungu vya 371 na 337 pamoja na kosa la kughushi kinyume na vifungu vya 333, 335(b) na 337 vya sheria ya kanuni ya adhabu [Cap 16 R.E 2002].

Kwa mujibu wa Kwariko, baada ya hukumu hiyo kutolewa, mtuhumiwa alitoroka bila taarifa kwa mahakama hali iliyosababisha TAKUKURU makao Makuu kuanza msako wa kumtafuta hadi alipokamatwa na kurejeshwa mahakamani manmo Machi 06, 2026

Amesema mahakama ilikataa utetezi wa mtuhumiwa kwa kuwa haukuwa na mashiko na hivyo hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Buhigwe akathibitisha hukumu ya kifungo cha miaka saba jela aliyopewa kwa makosa hayo manne

Related Posts