Morocco Watangazwa Mabingwa wa AFCON 2025, Senegal Wapokwa Ubingwa

CAF imeyabatilisha matokeo ya fainali na kuwapa Morocco ushindi wa 3 – 0. Bodi ya Rufaa ya CAF imetoa uamuzi kuwa Senegal ilipoteza fainali hiyo baada ya timu yake kuondoka uwanjani kulalamikia penalti waliyopewa Morocco. Sheria za CAF zinasema kuwa kama timu inakataa kucheza au kuondoka uwanjani basi inaondolewa mashindanoni.

Senegal iliifunga Morocco 1 – 0 katika fainali ya Januari 18 iliyogubikwa na tukio ambalo wachezaji wa Senegal waligoma kucheza baada ya wenyeji kupewa penalty ya dakika za majeruhi wakati mechi ikiwa sifuri sifuri. Baada ya mechi kucheleshwa kwa dakika 17, wachezaji wa Senegal kisha walirejea uwanjani na penalti iliyopigwa na Brahim Diaz ikaokolewa na kipa kabla ya Pape Gueye kufunga bao la ushindi katika muda wa ziada. BREAKING: Shirikisho la Soka la Senegal (FSF) limethibitisha kupokea uamuzi uliotolewa na Kamati ya Rufaa ya CAF kuhusu kupokwa ubingwa wa Kombe la Mataifa la Afrika 2025

FSF imepinga rasmi uamuzi huo ambao wanaona hauna msingi wa kisheria, upo kiholela na hauna uwiano. FSF inaamini kuna Ukiukaji mkubwa wa kanuni za kifungu cha 82 na 84 cha kanuni za CAF zilizohalalisha maamuzi hayo.

FSF imeeleza kuwa mwamuzi wa mechi hiyo alitumia uamuzi wake wa kuchagua kusimamisha mechi kwa muda na sio kusitisha kabisa. Mchezo ulianza tena, penati ilipigwa, na matokeo ya haki yalipatikana

Lakini pia wanaamini Utekelezaji wa kifungu cha 84 ni dhuluma. Wachezaji wa Senegal walirejea uwanjani na mwamuzi alithibitisha hilo, mechi ikaendelea hivyo kifungu cha 84 hakiwezi kufanya kazi

FSF imewaandikia barua CAF ikitaka wasimamishe utekelezaji wa uamuzi huu na kusitisha taratibu zote za kutoa kombe kwa Morocco ikisubiri usuluhishi wa mwisho lakini pia imeeleza nia yake ya kwenda kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) ndani ya saa 48 zijazo ili kutengua uamuzi huu.

Kwenye barua hiyo FSF imeomba kupata ripoti ya waamuzi na maafisa wa mechi hiyo ndani ya masaa 24, isipopata itafungua kesi ya dharula CAS

Related Posts