Mshtuko CAF ikiyafuta mashindano ya CHAN

Dar es Salaam. Jumamosi, Januari, 17, 2026 huenda ikabaki kuwa siku yenye kumbukumbu mbaya kwa wachezaji wanaocheza katika ligi za ndani barani Afrika.
Ni kufuatia uamuzi mgumu uliotangazwa na Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) wa kufuta Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN).

Uamuzi huo umetangazwa miezi mitano baada ya kufanyika kwa mashindano hayo yaliyoandaliwa kwa pamoja katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda ambapo Morocco iliibuka bingwa.

Lakini pia mashindano hayo yamefutwa baada ya kuishi kwa muda wa miaka 16, kwani yalifanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2009.

Rais wa CAF, Patrice Motsepe amesema kuwa sababu ya kufuta mashindano hayo ni kutokana na gharama kubwa ya fedha zinazotumika katika michuano hiyo.

“Hakutakuwa na CHAN. Hakuna haja ya kuwa na CHAN. CHAN ni tukio linalopoteza fedha nyingi kwa kiwango kikubwa,” amesema Motsepe.

Mashindano hayo yamefutwa huku timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ikiwa na historia ya kushiriki mara tatu tofauti ambazo ni mwaka 2009, 2022 na 2024.

Katika fainali za 2009 na 2022, Taifa Stars iliishia katika hatua ya makundi na katika fainali za 2024, ilifikia katika hatua ya robo fainali.

Wakati akitangaza kufutwa kwa CHAN, Motsepe amezihakikishia nchi za Tanzania, Kenya na Uganda kuandaa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

“Nina imani kubwa kwamba AFCON itakayofanyika Tanzania, Kenya na Uganda itakuwa na mafanikio makubwa sana. Ndiyo maana nilisisitiza CHAN ifanyike huko ili kuwaandaa. Hatutaiondoa AFCON ya 2027 kutoka Afrika Mashariki. Timu itaenda huko Jumatatu kuanza ukaguzi wa kina,” amesema Motsepe.

Related Posts