Watumishi watatu wa kada ya afya akiwamo Mganga Mkuu wa Wilaya ya Urambo mkoani Tabora wamesimamishwa kazi huku wengine wawili wakiendelea kuhojiwa kufuatia tuhuma za kubakwa kwa mgonjwa na mmoja wa matabibu wa Hospitali ya Wilaya ya Urambo katika mchakato wa kupatiwa matibabu.
Tukio hilo lilitokea Novemba 24,2025 katika Hospitali ya Wilaya ya Urambo ambapo tabibu huyo (Juma Selemani) anaelezwa kufanya ubakaji huo kwa madai ya kwamba anamuwekea dawa ya kusafisha njia ya uzazi.
Desemba 01, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paulo Chacha akiongozana na Kamati ya Usalama ya Mkoa amefika hospitalini hapo na kutoa maagizo ya kusimamishwa kazi kwa watumishi katika mkasa huo pamoja na mambo mengine ya uzembe kazini kwa baadhi ya watumishi.
Akizungumza na Kamati ya Usalama na watumishi hospitalini hapo, RC Chacha amesema Mganga Mkuu wa Wilaya ya Urambo Dkt. David Manyama aliunda tume maalumu hospitalini ili kuficha ukweli wa jambo hilo hali iliyomfanya Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora Dkt. John Mboya kuunda pia tume ya uchunguzi wa suala hilo mpaka pale ukweli ulipobainika.

