Mwanasheria Mkuu Mpya Atangaza Kumsaka Mange Kimambi

Dar es Salaam — Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza kuwa itahakikisha inamkamata mwanaharakati wa mitandaoni, Mange Kimambi, ambaye ni Mtanzania anayeishi nchini Marekani, kwa madai ya kuhamasisha na kuchochea vurugu zilizotokea nchini kuanzia Oktoba 29, 2025.

Kauli hiyo imetolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Hamza Johari, muda mfupi baada ya kuapishwa rasmi na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 5 Novemba 2025, kuendelea kuongoza ofisi hiyo nyeti serikalini.

Amesema serikali haitakubali kuona mtu mmoja akiwa nje ya nchi anatumia mitandao ya kijamii kuvuruga amani na kuathiri utulivu wa taifa, kisha baadaye kuonyesha majivuno kana kwamba yupo juu ya sheria. Mwanasheria Mkuu huyo alisisitiza kuwa vitendo hivyo ni vya dhihaka na kudharau mamlaka ya nchi, hivyo hatua kali lazima zichukuliwe.

“Haiwezekani mtu anakaa nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, halafu anawaambia watu wafanye vurugu, na wanafanya kweli. Kisha baadaye anajisifia hadharani kwamba bado atarudi kivingine — hilo haliwezi kuvumiliwa,” alisema Johari kwa msisitizo.

Ameeleza kuwa pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kufuatilia suala hilo kwa karibu, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu nayo itashiriki kikamilifu kuhakikisha taratibu zote za kisheria zinafuatwa katika kufanikisha kumfikisha Mange Kimambi mbele ya vyombo vya dola.

Johari aliongeza kuwa vurugu zilizohamasishwa mtandaoni zimesababisha uharibifu mkubwa wa mali za umma na binafsi, ikiwemo gari la ofisi yake binafsi ambalo limechomwa moto wakati wa machafuko hayo. Alisema dereva wake alinusurika kwa kukimbia, jambo linaloonyesha ukubwa wa madhara yaliyotokana na vitendo hivyo vya uchochezi.

“Tumeona mali za watu binafsi zikiharibiwa, tumeona magari ya serikali yakiteketezwa kwa moto, ikiwemo gari la Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Haiwezekani taifa kukaa kimya mbele ya matukio kama haya,” alieleza kwa ukali.

Serikali imesisitiza kwamba haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya yeyote anayejaribu kuvunja amani, kuchochea ghasia, au kupandikiza chuki kupitia mitandao ya kijamii, na kwamba Tanzania itaendelea kuwa nchi ya amani na utulivu kwa wananchi wake wote.

Related Posts