Waziri Mkuu wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amelaani vikali tabia ya baadhi ya watu kueneza taarifa za uongo na zisizofanyiwa uchunguzi, akisema hatua hiyo imefika kiwango cha kuwaumiza na kuwavuruga wananchi.
Akizungumza leo, Novemba 21, 2025, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Bombadia, Halmashauri ya Singida Mjini, Dkt. Mwigulu amesema Watanzania “wamefikwa pabaya” kutokana na kuaminisha taarifa zisizo sahihi bila kuzichuja.
“Tumefikishwa pabaya sana. Watu wamejipa haki wao, wamekuwa ndugu zake na Mungu, ni ‘wakweli’, na wengine wote nyie ni waongo, ni wabaya. Mmefikishwa pabaya Watanzania, na kila jambo mmeanza tu kubeba (kuamini),” alisema.
Ameongeza kuwa hivi sasa watu hawana woga hata wa kusingizia mambo ambayo hawana uhakika nayo. Ametoa mfano wa taarifa zilizoenea mitandaoni zikidai kuwa magari yaliyoteketezwa hivi karibuni ni mali ya mke wake, Ester, ambaye imedaiwa kuwa ni jina la magari hayo.
“Siku hizi watu hawaogopi hata kusingizia watu. Anasingizia akiwa mkavu, hafanyi hata utafiti wa kumjua vizuri mtu anayetaka kumsema. Juzi nikasikia tumechoma magari ya Ester, ya Mbunge wa Iramba (Mwigulu Nchemba). Eti ni magari yake yanaitwa Ester, jina la mke wake. Mke wangu haitwi Esther, anaitwa Neema, na leo nilikuwa naye,” amesema.
Akiendeleza ufafanuzi, Dkt. Mwigulu amekanusha pia madai kuwa mali hiyo huenda inahusiana na mama yake.
“Wanasema, ‘aa basi kama siyo ya mke wake, itakuwa ya mama yake.’ Mama yangu ni binti wa Kiislamu anaitwa Asha Ramadhan Omary. Hamumjui? Yupo hapa,” amesisitiza.
Mkutano huo umefanyika kwa lengo la kumpongeza na kumpokea Dkt. Mwigulu baada ya kuapishwa kwake kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania.

