Nature

Mwigulu “Vifo vya Watu Mnataka Tuhesabu Kama Magari Haiwezekani”

Serikali ya Tanzania imethibitisha kutokea kwa vifo katika maandamano ya siku ya uchaguzi ya Oktoba 29, 2025, na siku zilizofuatia. Hata hivyo, imeonya dhidi ya kuhesabu idadi ya waliopoteza maisha kama “magari,” ikisema kufanya hivyo kunapunguza utu na kuongeza maumivu kwa familia zilizoondokewa na wapendwa wao.

Waziri Mkuu wa Tanzania, Mwigulu Nchemba, amesema haifai kwa watu kuzungumzia idadi ya vifo kwa namna ya kupunguza hadhi ya maisha ya binadamu.

“Tukakiri, vurugu hizi zimepoteza maisha ya watu. Lakini mnataka tuhesabu kama magari? Maisha ya watu mnataka tuhesabu kama magari?”

Akiendelea kusisitiza thamani ya maisha ya binadamu, Mwigulu alitolea mfano jinsi watu wanavyozungumzia vifo kwa wepesi:

“Hivi unajua damu ya binadamu ilivyo? Wanaongelea eeh elfu ngapi, sijui elfu ngapi, sijui laki ngapi… tuwe makini. Kuna vita ya kiuchumi.”

Akizungumza Novemba 25 katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habari, Waziri Mkuu alionya kuwa hakuna nchi duniani ambayo vurugu hutokea bila madhara. Alitoa wito kwa taifa kuchagua majadiliano na maridhiano badala ya misuguano.

“Duniani kote hakuna vurugu zinatokea zisizokuwa na madhara. Pakiwapo vurugu, patakuwa na madhara. Kuna watu wamepoteza wapendwa wao tujiepushe kufanya hili kama mchezo au siasa.”

Akizungumzia uvumi wa maandamano mengine yanayotajwa na mitandao kufanyika Desemba 9, Waziri Mkuu alisisitiza umuhimu wa kuepusha taifa kuingia kwenye misukosuko mipya, akihimiza majadiliano kama njia ya kutatua changamoto.

“Natoa rai kwa Watanzania: Tukae tukajadili kuona wapi palipo na changamoto. Tusiruhusu tena jambo la aina hiyo. Hakuna vurugu isiyokuwa na gharama ina makovu, ina gharama za uhai.”

Aidha, alisema vyombo vya ulinzi vina wajibu wa kikatiba kulinda usalama wa raia na mali zao, lakini akasisitiza kuwa raia wenye malalamiko wanapaswa kutumia njia zisizochochea machafuko.

“Wenye machungu waone njia nyingine, si kuturudisha kwenye vurugu. Ni hatari kwa taifa tukizoea kufikiria kuwa kila jambo linapotokea ni jukumu la vyombo vya dola.”

Maandamano ya siku ya uchaguzi Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuatia yamesababisha vifo vya watu kadhaa, majeruhi, kupotea kwa watu, na uharibifu mkubwa wa mali. Haya yameliweka taifa hilo katika macho ya kimataifa, yakitajwa kama miongoni mwa maandamano makubwa zaidi kuhusu uchaguzi tangu Tanzania kupata uhuru zaidi ya miongo sita iliyopita.

Maandamano hayo yalianzia Dar es Salaam na kusambaa hadi miji mingine kama Arusha, Mwanza, Mbeya, Dodoma na mikoa mingine, yakiharibu ofisi za serikali, ofisi za chama tawala (CCM), vituo vya mafuta, vituo vya polisi, pamoja na maduka ya wananchi.

Hadi sasa, serikali bado haijatoa tathmini rasmi ya madhara kamili ya maandamano hayo, huku Rais Samia Suluhu Hassan akiunda Tume ya kuchunguza, iliyopewa miezi mitatu, tume ambayo hata hivyo inakosolewa na vyama vya upinzani, wakiitaja kukosa uhalali wa uhuru kutokana na madai kwmaba baadhi ya wajumbe wananyooshewa kidole kwa uvunjivu wa haki za binadamu.

Related Posts