
Mgombea Mwenza wa Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Emmanuel Nchimbi, amemuomba aliyekuwa Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, kurejea kwenye chama chake cha awali CCM na ameahidi atampokea mwenyewe kwa mikono miwili endapo atarudi.
Akizungumza Septemba 2, 2025, akiwa katika mchakato wa kuzisaka kura Jimbo la Kisesa, mkoani Simiyu, Nchimbi amesema Mpina hana budi kurudi nyumbani CCM kwa kuwa bado ni sehemu ya familia hiyo ya kisiasa.
“Atakayempigia simu Mpina amwambie kaka yake mkubwa alipita hapa. Mwambieni hasiponipigia kura atakuwa amekosa adabu ya Kisukuma kabisa, maana nilipopita si aliwaambia kwamba mimi kaka yake. Mwambie kaka yako alipita hapa na anasubiri. Akirudi tena, anataka urudishe hiyo kadi ya chama chako kipya, urudi CCM na mimi nitapokea kadi ya Mpina mwenyewe, simtumi mtu yoyote,” amesema Nchimbi.
Mpina, ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Kisesa kwa tiketi ya CCM, alihama chama hicho baada ya kushindwa kwenye kura za maoni na kujiunga na ACT-Wazalendo, ambako aliteuliwa kugombea Urais. Hata hivyo, msajili wa vyama vya siasa alimzuia kuendelea na kinyang’anyiro hicho baada ya mwanachama wa ACT, Monalisa Ndala, kufungua malalamiko akidai kuwa hakutimiza vigezo vya kugombea. Suala hilo kwa sasa linaendelea Mahakamani.

