Watu 95 wamepandishwa kizimbani jioni ya leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka mawili ikiwemo uhaini.
Washtakiwa hao wanafanya jumla ya watu waliofikishwa mahakamani hapo kwa siku ya leo ambao wanakabiliwa na kesi za uhaini kuwa 240 ikiwemo Mfanyabiashara Jenifer Jovin (Niffer)
Watuhumiwa hao wamesomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkuu, Hassan Makube ambaye ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 19, 2025 kwa ajili ya kutajwa.
Awali wakisomewa mashtaka yao, idaiwa kuwa kati ya Aprili Mosi, hadi Oktoba 29,2025 wanadaiwa walikula njama na kupanga kwa siri kufanya kosa la uhaini.
Pia shitaka la pili washitakiwa wote ilidaiwa Oktoba 29, 2025, katika maeneo Sinza ndani ya jiji la Dar es Salaam, wakiwa chini ya utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku wakiwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, waliunda nia ya kuzuia Uchaguzi Mkuu wa 2025 kwa kutishia mamlaka na kusababisha uharibifu wa mali za serikali.
Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo. Kesi haina dhamana.

