Nature

Padri Kitima Aweka Wazi Sababu za Kikao Chake na Waziri Mkuu

Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Novemba 20, 2025 alikutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima, katika Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dkt. Charles Kitima, ameeleza kwa uwazi kuwa kikao chake na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, kilichofanyika Novemba 20, 2025, katika Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam, kilikuwa cha binafsi na hakikuwakilisha mazungumzo ya Baraza la Maaskofu.

Akizungumza na wanahabari Jumatatu, Desemba 1, 2025, Padri Kitima alibainisha kuwa alikwenda katika mazungumzo hayo kufuatia mwito wa binafsi kutoka kwa Waziri Mkuu, na si kama mwakilishi wa TEC.

Amesisitiza kuwa hakupokea barua, ajenda wala maelekezo yoyote kutoka TEC kabla ya kwenda katika mazungumzo hayo, jambo linalothibitisha kuwa hakutumwa na taasisi.

“Waziri Mkuu alinipigia simu yangu binafsi na kuniambia angependa tuzungumze kama watu wanaofahamiana. Tumekuwa na uhusiano mzuri kwa muda mrefu,” alisema Padri Kitima.

Ameeleza kuwa katika mazungumzo yao waligusia kwa ujumla matukio yaliyotokea baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, lakini mazungumzo hayo yalikuwa katika muktadha wa kibinadamu na si wa kitaasisi.

Padri Kitima amefafanua kuwa kama kungekuwepo haja ya mazungumzo rasmi kwa niaba ya Baraza la Maaskofu, basi angefuata utaratibu wa kupata kibali kutoka kwa Rais wa TEC, ambaye ndiye msemaji na mwenye mamlaka ya kutoa misimamo rasmi ya baraza.

Related Posts