
Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imebaini kuwepo kwa taarifa zisizo sahihi zinazosambazwa mitandaoni kuwa kila mwenye kamera za usalama (CCTV) anatakiwa kujisajili na Tume hiyo.
Kupitia ufafanuzi wake, Tume imeeleza kuwa si kweli kwamba kila mtu binafsi mwenye kamera za CCTV anatakiwa kujisajili.
Kwa mujibu wa sheria, wajibu wa kujisajili unawahusu taasisi zote za umma na binafsi zinazokusanya au kuchakata taarifa binafsi, ikiwemo kupitia matumizi ya CCTV, na siyo kila mtu mmoja mmoja. Taasisi hizo zinapaswa kujisajili na Tume kabla au ifikapo Aprili 8, 2026.
Kwa upande wa matumizi ya CCTV katika makazi binafsi, Tume imeelekeza kuwa kamera zinapaswa kuelekezwa ndani ya mipaka ya eneo la mhusika pekee. Imeonya kuwa iwapo kamera zitarekodi maeneo ya nje ya mipaka hiyo, hususan maeneo ya umma, matumizi hayo yatakuwa kinyume cha sheria na mhusika atawajibika kwa mujibu wa sheria.
Aidha, Tume imesisitiza umuhimu wa kuweka alama maalum (signage) zinazoonesha kuwa eneo husika lipo chini ya uangalizi wa CCTV inayokusanya taarifa binafsi, ili kulinda faragha za watu.
PDPC imeeleza kuwa itaendelea kutoa miongozo zaidi ili kuhakikisha matumizi sahihi ya teknolojia ya CCTV yanafuata sheria na kulinda haki za faragha za wananchi.
