Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama, amesema jeshi hilo linaendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika Makanisa ya Ufufuo na Uzima yanayoongozwa na Askofu Josephat Gwajima yaliyopo mkoani humo.
Akizungumza kwa njia ya simu na kituo kimoja cha habari, RPC Mkama alieleza kuwa bado kuna zuio la Serikali dhidi ya shughuli za makanisa hayo, na kwamba jeshi lake linaendelea kulisimamia kwa mujibu wa sheria.
“Bado tunalinda, na walijaribu kuja watu huko maeneo ya Kanisa la Ufufuo Kihonda, lakini tumewaelimisha waumini hao kuwa eneo hilo bado lina katazo la Serikali. Hayo yanayoendelea kwenye mitandao ya kijamii, sisi hatujapewa tamko lolote la kulifungua kanisa,” alisema Kamanda Mkama.

