
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amekutana na kuzungumza na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, tarehe 27 Agosti, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, leo tarehe 27 Agosti 2025, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.

Mazungumzo hayo yalihusu masuala mbalimbali yanayohusiana na sekta ya sheria nchini, ikiwemo nafasi ya wanasheria katika kukuza demokrasia, utawala wa sheria, na haki za wananchi.
Ikulu imesema kikao hicho ni sehemu ya jitihada za Serikali kuendelea kushirikiana na wadau wa kisheria kwa ajili ya kuimarisha misingi ya haki na uwajibikaji nchini.
Boniface Mwabukusi Ameandika Haya:
Leo nimefika Ikulu ya Chamwino kuwasilisha majumuisho ya wadau mbalimbali, ambapo tulipata nafasi adhimu ya kuzungumza na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwasilisha kwa Mukhtasari kuhusu masuala makuu ya kitaifa yanayohusu:
- Utawala Bora na Demokrasia – tukisisitiza umuhimu wa kuweka mifumo thabiti inayohakikisha heshima ya utawala wa sheria, uwajibikaji na uwazi.
- Haki za Ushiriki katika Chaguzi tukieleza haja ya kuwa na uchaguzi unaozingatia haki za wananchi, ushiriki huru wa wagombea, na kuondoa vikwazo vya kiufundi vinavyoweza kunyima wananchi na wagombea haki ya kidemokrasia.
- Changamoto za Utekaji na Kutoweka kwa Watu (Enforced Disappearances) tukimueleza Mheshimiwa Rais juu ya umuhimu wa kulinda haki za msingi za raia kwa kuzuia vitendo hivi visivyo vya kisheria.
- Maboresho ya Mfumo wa Uchaguzi tukihimiza mageuzi yatakayowezesha chaguzi zilizo huru, haki na shirikishi, ili wananchi wapate viongozi wanaowataka kupitia sanduku la kura bila hila wala vizuizi visivyo halali na kuondoa changamoto ya kukata wagombea au kuzuia Mawakala.
- Suala la Mh.Tundu Lissu tuliliwasilisha kwake na linaendelea kuangaliwa na kufanyiwa kazi kwa utaratibu mwingine lakini bila kuingilia kinachoendelea Mahakamani
Mheshimiwa Rais alitusikiliza kwa makini na akatoa ahadi ya kuangalia kwa karibu mapendekezo yaliyotolewa, ili kuona namna bora ya kuyatekeleza kadri muda na mazingira yanavyoruhusu.
Aidha, kwa kuwa mapendekezo hayo yamegawanyika katika ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu, Mheshimiwa Rais ameahidi kuyapitia kwa ukamilifu na kuchukua hatua stahiki kwa yale yatakayowezekana, ili kuhakikisha Taifa linaingia kwenye uchaguzi ulio bora zaidi, wenye heshima, uhuru na haki kwa Watanzania wote.
BAK MWABUKUSI

