Rais Samia Ataja Sababu Kwanini Kamchagua Mwigulu Kuwa Waziri Mkuu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema uteuzi wa Dk. Mwigulu Nchemba kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania umefanyika kwa kuzingatia vigezo vingi na ushindani mkali miongoni mwa majina yaliyowasilishwa kwake, na kwamba Dk. Mwigulu ameibuka kinara kutokana na sifa na uwezo alioonesha katika utumishi wa umma.

Akizungumza Ijumaa, Novemba 14, 2025, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma mara baada ya kuapishwa kwa Dk. Nchemba, Rais Samia alisema kwamba hatua hiyo imekuja baada ya tathmini ya kina kufanywa kuhusu uzoefu na mchango wa wagombea wote waliopendekezwa. Alisema kuwa moja ya sababu kubwa zilizopelekea kumteua Dk. Mwigulu ni uzoefu wake wa muda mrefu katika kuwahudumia wananchi wa Tanzania kupitia nafasi mbalimbali za uongozi serikalini.

Rais Samia alibainisha kuwa utumishi wa Dk. Mwigulu ndani ya Wizara ya Fedha ulimjengea uwezo wa kipekee wa kufahamu mifumo ya upatikanaji na usimamizi wa fedha za Serikali—jambo ambalo ni muhimu katika kuratibu utekelezaji wa majukumu ya wizara na taasisi mbalimbali za Serikali. “Vigezo vyote tulivyopima, tulipima katika maeneo tofauti ya kuitumikia nchi hii. Kipaumbele chetu ni kupata mtu anayejua namna ya kuwatumikia wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia aliongeza kuwa kutokana na uzoefu huo, anaamini Dk. Mwigulu atakuwa msaada mkubwa katika kuratibu shughuli za serikali, kusimamia bajeti, pamoja na kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo unaenda kwa kasi na ufanisi.

Kwa upande wake, Dk. Mwigulu ameahidi kufanya kazi kwa bidii, ushirikiano na uadilifu, huku akiahidi kuendelea kutanguliza maslahi ya wananchi katika utendaji wake wa kila siku. Wengi wameelezea uteuzi huo kama hatua muhimu inayoweza kuleta msukumo mpya katika serikali, hasa kipindi hiki ambacho taifa linahitaji uthabiti wa kiuchumi na kisiasa.

Kwa ujumla, uteuzi huu umepokelewa kwa hisia tofauti lakini wengi wakitarajia kuwa ujuzi na uzoefu wa Dk. Nchemba utaleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Related Posts