
Mwamuzi wa Kati wa mchezo wa #MtibwaSugar dhidi ya #Yanga (Machi 21, 2026), Gilbert Mrina kutoka Kilimanjaro ameshushwa Daraja la Uamuzi kwa kushindwa kuchukua hatua stahili kwa mchezaji Djigui Diarra wa Yanga aliyeonesha utovu wa nidhamu (kumshambulia Mwamuzi) kama ilivyoainishwa katika Kanuni ya 42:1(1.6) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.
Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeeleza ni kosa la kujirudia ambapo Gilbert Mrina alitenda kosa la aina hiyo katika mchezo Mbeya City vs Namungo (Ligi Kuu), akafungiwa mizunguko mitatu.
Pia, Mwamuzi Msaidizi namba mbili wa mchezo huo, Abdulaziz Ally kutoka Arusha amefungiwa mizunguko mitano kwa kushindwa kutafsiri vema Sheria za Soka, dakika ya 36 alinyoosha kibendera juu kuashiria Emmanuel Mwanengo wa Yanga ameotea wakati haikuwa hivyo.
