
Jeshi la Polisi Mkoani Arusha limesema linaendelea kufanya uchunguzi kuhusu tukio la Mwanafunzi wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Sombetini kudaiwa kujeruhiwa kwa risasi na inadaiwa kuwa risasi hiyo ilifyatuliwa na Mgombea Udiwani wa Kata ya Sombetini, Abdullazizi Chende maarufu kwa jina la Dogo Janja, wakati akijaribu kujihami alipokuwa akishuka kwenye gari lake baada ya kutaka kuvamiwa na kijana huyo pamoja na wenzake.
Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi leo August 25, Chende alitumia silaha aliyokuwa nayo baada ya kuhisi anaweza kushambuliwa, hata hivyo, ndugu wa kijana huyo pamoja na baadhi ya wakazi wa eneo hilo wamekanusha madai kwamba kijana huyo alikuwa mhalifu.
Mashuhuda wa eneo hilo wametaja kuwa mara nyingi kijana huyo huonekana akiishi kwa amani na familia yake na siku ya tukio alielekea nyumbani kwa ajili ya chakula, baadhi ya Wananchi walioshuhudia walisema walihisi kijana huyo alidhulumiwa kwani hakuna rekodi za awali zinazomuhusisha na vitendo vya kihalifu.
Baada ya tukio, kijana huyo alipelekwa hospitali kupata matibabu huku Polisi wakiendelea na upelelezi zaidi na familia ya kijana huyo na baadhi ya viongozi wa Mtaa wametoa wito wa haki kutendeka, wakisisitiza kuwa kijana huyo hakuwa Jambazi kama ilivyodaiwa awali.

