Bwana Yesu Asifiwe…. Asalaam Alaykum!
Nimefanikiwa kuona hotuba ya ndugu Majizzo, kwa mtazamo wangu nadhani ni hatua nzuri ya kufungua mazungumzo ya yale ambayo kwa muda sasa yamekua wazi ila kama ni “MWIKO” kuyazungumzia, hasa kwa upande wa wasanii.
Ni mengi tunaweza kusema ila tunapoamua kusema tukumbuke tunaongea na akina nani…. Tunaongea na Taifa ambalo linalia, linavuja damu na liko kwenye msiba endelevu…
Tunaongea na watu ambao wamezika WATOTO wao, BABA zao, MAMA zao na ndugu, jamaa au marafiki. Wengine wamezika NGUO na wengine hawajui kama wapendwa wao wapo hai au wamekufa. Tunaongea na watu ambao wengi hawana uwezo wa kupata elimu au kuwaelimisha watoto wao, wengine hawana uwezo wa kupata huduma za afya na wengi wana magonjwa yasiyotibika. Na tunapoomba support kwa watu hawa, tukumbuke tunaomba kulindiwa ajira zetu na watu ambao HAWANA AJIRA.
Kulinda ajira ni hoja aliyoizingatia sana ndugu Majizzo, ila tunaanzaje kulinda ajira kabla ya kulinda MAISHA kwanza? Tunawaombaje watu wasiokua na uhakika wa kuishi watushike mkono tuendelee kula maisha?
Ni wakati sasa tujiulize tunarudishaje huo mkono wa support kwa shabiki zetu na jamii kiujumla! Pale tulipokosea tusiseme “yamepita basi yaishe, tuendelee tulipoishia” maana uchafu ukiuficha chini ya zulia utazaa funza na maradhi ya baadae. Tusiwape mashabiki mizigo yote ya kubeba maumivu na kutubeba na sisi pia, hata baada ya kuwakosea. Tujiulize tunawezaje kukiri na kuwajibika kwa kubadili mwenendo bila kuwa na sababu za kujiridhisha kiuchumi
Ni dhahiri sasa hivi Taifa limeshika tama, na haitoshi kusema “Poleni kwa wafiwa” na kuendelea kuzungumza agenda zingine bila kuzingatia UPONYAJI, UKWELI na HAKI kupatikana!
Rosa MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU IBARIKI AFRIKA✊🏾
