Rais wa Kenya William Ruto ameupinga wito na kampeni inayoendelea kwa kasi nchini humo ya “Ruto Must Go” akisema kuwa hakuna haja ya kushinikiza kwani muda wake wa kuondoka ukifika ataondoa na ataachia Madaraka.
Ruto ameyasema hayo wakati akihutubia katika Soko la Hisa la Nairobi (NSE) hii leo julai 23, 2025 ambapo amesema kuwa hakuna kiongozi wa nchi hiyo ambaye amewahi kumaliza muda wake akaendelea kusalia madarakani.
“Kama wale waliokuwa kabla yangu wameondoka, wakati wangu utafika na nitaendaLakini, kwa heshima, mabwana na mabibi, ni sababu gani zenu zinawafanya mseme ‘Ruto lazima aondoke’? Labda hukubaliani na sera na mipango Ruto aliyo nayo kwa taifa, ambayo ni sawa. Lakini tafadhali, ungetupendelea kwa mpango wako mbadala? Kadiri ninavyosikiliza, ndivyo ninavyoona ni porojo tu.” amesema Rasi William Ruto
Aidha amesema kuwa wanaharakati na viongozi wanaotaka kumtoa madarakani walete mpango mbadala huku akisema kuwa “Huwezi kubadilisha mpango usioupenda bila chochote… Nimesikia wengine wakisema, Mwache Ruto na tutatafuta mpango mbadala baadaye Kwangu mimi huo unaonekana kama ulaghai wa ‘safisha safisha” akirejela shughuli za ulaghai zinazoendelea nchini humo.
Tangu Ruto aingie madarakani kumeshuhudiwa kiwepo kwa maandamano ya mara kwa mara yanayoongozwa na vijana dhidi ya utawala wake na hii baada ya kampeni zake wakati wa uchaguzi ambapo aliahidi kupunguza gharama za maisha kwa Wakenya wa kawaida kitendo ambacho waandamanaji wengi wamesema ameshindwa kukitimiza wakimtaka aondoke madarakani.

