Simba: Hatujagawa Utamu Mara Mbili kwa Mpinzani Mmoja

DAR ES SALAAM : SIMBA imesema haitakubali kupoteza mara mbili dhidi ya mpinzani mmoja, ikiahidi kupambana hadi mwisho kuhakikisha inapata ushindi dhidi ya Stade Malien katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa Februari 14 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, Msemaji wa Simba, Ahmed Ally, amesema kikosi hicho kimejipanga kurejesha heshima na kuondoa dhana iliyojengeka kwa mashabiki kwamba hakiwezi kushinda kwenye Uwanja wa Mkapa msimu huu.

“Msimu huu hatujapata ushindi wowote kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa katika Ligi. Matokeo haya yamefanya imani imewapotea Wanasimba ya kupata ushindi kwenye uwanja huo. Sasa tunakwenda kufuta hii dhana, tunakwenda kurudisha imani kwamba kwa Mkapa ni nyumbani kwetu na tunaweza kushinda,” amesema.

Amesisitiza kuwa ni falsafa ya Simba kutoruhusu kupoteza mara mbili kwa mpinzani yuleyule, akitoa mfano wa michezo ya nyuma dhidi ya Al Ahly na Petro ambapo walijibu mapigo walipokutana tena nyumbani.

Hata hivyo, Ahmed amekiri kuwa licha ya ushindi wowote utakaopatikana kutokubadili hatma yao ya kufuzu, mchezo huo ni muhimu kwa ajili ya kurejesha hali ya kujiamini kwa wachezaji kuelekea mashindano ya ndani.

Amewataka Wanasimba kujitokeza kwa wingi uwanjani Februari 14 kuishangilia timu yao licha ya kushindwa kufuzu robo fainali msimu huu.

“Tukubali kiroho safi kwamba mwaka huu tuliteleza. Hakuna Mwanasimba anatakiwa kubaki nyumbani siku hiyo. Twendeni tukawape ujumbe wachezaji wetu kwamba bado tupo pamoja nao,” amesema.

Ahmed pia amewataka mashabiki kuepuka kuwatukana viongozi au kuleta mpasuko ndani ya klabu kutokana na matokeo ya msimu huu.

“Ni kawaida kwenye maisha, kuna muda unafanya vizuri na kuna muda unateleza. Ukishindwa unakaa chini na kujipanga kwa msimu ujao,” alisema.

Katika hatua nyingine, alitangaza viingilio vya mchezo huo kuwa ni kama ifuatavyo: Mzunguko Sh3,000; VIP C Sh5,000; VIP B Sh10,000; VIP A Sh20,000 na Platinum Sh100,000.

Kwa mujibu wa Ahmed, wapinzani wao Stade Malien wanatarajiwa kuwasili nchini Februari 13 alfajiri na kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya mchezo wa Februari 14.

Related Posts