‘DO or Die’ ndicho kitu pekee wanachohitaji Simba ili kuvuka makundi na kuingia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu wa 2025-26.
Baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Esperance ya Tunisia, ‘Wekundu wa Msimbazi’ wako mkiani mwa Kundi D.
Si tu mkiani, bali pia hawajakusanya pointi hata moja baada ya kufungwa mechi zote tatu katika Kundi lao hilo linaloongozwa na Stade Malien ya Mali yenye pointi saba.
Esperance wako nafasi ya pili wakiwa na pointi tano, wakifuatiwa na Petro de Luanda waliokusanya pointi nne.
Kilichoiangusha Simba katika mechi tatu zao si tu ubutu wa safu ya ushambuliaji, ambayo imefunga bao moja pekee, bali pia ‘ukuta’ wao umeruhusu mabao manne.
Kwa hesabu zilivyo, vigogo hao wa Ligi Kuu Bara wamebakiza mechi tatu kwenye Kundi, ambapo ni dhidi ya Esperance, Stade Malien na Petro.
Kuziweka sawa hesabu, Simba watacheza nyumbani dhidi ya Esperance na Malien, huku wakiwa na mtihani mgumu wa kuifuata Petro nchini Angola.
Kwamba kama ‘Do or Die’ itafanya kazi, basi watajihakikishia pointi tisa, ambazo ni wazi zitatosha kuwapelekea hatua inayofuata (robo fainali).
Timu mbili za kila kundi zitavuka hatua ya makundi. Kufanikisha hilo, benchi la ufundi la Wekundu wa Msimbazi hao linapaswa kuzifanyia kazi kasoro zilizojitokeza katika mechi tatu zilizopita.
Ikimaanisha, safu ya ulinzi na ile ya ushambuliaji zinapazwa kuwa na ubora wa kutosha kuisaidia Simba kufaulu mtihani mgumu huo.
