Nature

Stars Yatoa Onyo CHAN

WAKATI Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ikitoa onyo kuelekea michuano ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Uganda (Uganda Cranes), kwenye mechi ya CECAFA 4 Nations, Watanzania wametakiwa kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Benjamin Mkapa Agosti 2, mwaka huu, kuiunga mkono dhidi ya Burkina Faso.

Stars itashuka uwanjani hapo kuikaribisha Burkina Faso ikiwa ni mechi ya ufunguzi ya michuano ya CHAN, ambayo inafanyika kwa ushirikiano wa nchi tatu; Tanzania, Kenya na Uganda.

Hayo yalisemwa jana na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, wakati akizindua kampeni ya hamasa kuelekea michuano hiyo, iliyofanyika Mbagala Zakhiem, Dar es Salaam.

“Ninaomba Watanzania mjitokeze kwa wingi siku hiyo ili kuishangilia timu yetu ya taifa tuna kikosi chenye wachezaji wenye uwezo mkubwa naamini Kombe la CHAN litabaki nyumbani,” alisema Mwinjuma.
Naibu Waziri huyo alisema serikali imejipanga vizuri kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri katika mchezo huo wa ufunguzi kwa kujenga na kuboresha miundombinu mbalimbali ya viwanja.

Kwa upande wa Ofisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Charles Maguzu, alisema ni wakati wa Watanzania kuchangamkia kila fursa katika kipindi chote kwa kuongeza uchumi kupitia mashindano hayo.

Alisema fursa hizo ni kwa wafanyabiashara wanaotoa huduma za kijamii zikiwamo hoteli, wasafirishaji pamoja na wafanyabiashara.

Msemaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Cliford Ndimbo, alitangaza viingilio vya mchezo huo kuwa ni VIP A Sh. 10,000, VIP B na VIP C Sh. 5000 huku mzunguko ikiwa ni Sh. 2,000.

“Tumetoa viingilio rafiki ili kila mmoja apate nafasi ya kuingia uwanjani kuishangilia timu yetu ya taifa ambapo mwaka huu tumekuwa na kaulimbiu ya ‘Linabaki Nyumbani'”, alisema Ndimbo.
Kwa upoande wa mchezo wa jana wa CECAFA 4 Nations, bao pekee lililofungwa na winga, Idd Selemani ‘Nado’, dakika 14, liliipa ushindi wa 1-0, Taifa Stars dhidi ya Uganda Cranes, ikitoa onyo kwa timu zote zinazoshiriki fainali za CHAN, kwani imeonesha kuwa imejipanga na ipo imara.

Stars ilipata ushindi wa kwanza katika mchezo wa CECAFA 4 Nations, uliochezwa Uwanja wa Black Rhino, Karatu, Arusha.

Michuano hiyo ni maalum kwa ajili ya kuzipa mazoezi timu wenyeji wa fainali hizo za CHAN zinazotarajiwa kuanza kutimua vumbi kuanzia Agsoti 2, hadi Agosti 30, mwaka huu, nchini hapa Uganda na Kenya.

Hata hivyo, Timu ya Taifa ya Kenya, Harambee Stars, imejitoa kwenye michuano hiyo ya CECAFA, badala yake zimesalia timu tatu tu, ambazo ni Stars, Uganda Cranes na Senegal, ambayo ni timu alikwa.

Nado aliupata mpira nje kidogo ya eneo la hatari, akageuka na kuingia nao ndani kabla ya kupiga shuti la chini kwa mguu wa kushoto, lililombatiza kipa Joel Mutakubwa, akiwa katika juhudi za kuokoa, ukajaa wavuni.

Abdul Selemani Sopu, angeweza kuipatia Stars bao la pili, dakika ya 37, kama mpira alioupiga kwa mguu wake wa kushoto usingepaa juu ya lango, akiwa anatazamana ana kwa ana na kipa Mutakubwa.

Alikuwa amepata pasi kutoka kwa Nassor Saadun, ambaye naye alipasiwa na Feisal Salum, aliyewanyang’anya mabeki wa Uganda ambao walikuwa wakipasiana karibu na lango lao.

Hata hivyo, katika purukushani hizo, mchezaji huyo aliumia kwani baada ya kuupiga, alikutana na daluga kutoka kwa Helbert Achani. Sopu alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Jammy Simba, anaichezea, JKU ya Zanzibar.

Nusura Uganda Cranes isawazishe dakika moja kabla ya mapumziko, baada ya kona iliyopigwa kutua kwenye kichawa na Jude Ssemugabi, lakini kipa Yacoub Suleiman alikaa imara na kudaka mpira huo uliokuwa unaelekea wavuni.

Kipindi cha pili kilitawaliwa zaidi ya Waganda ambao waliliandama lango la Stars kama nyuki, lakini mabeki, Shomari Kapombe, Paschal Msindo, Dickson Job, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, pamoja na Wilson Nangu na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ waliongia kipindi cha pili, walikaa imara wakiongozwa na kipa, Yacoub Suleiman kuokoa hatari nyingi za Uganda Cranes.

Related Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *