Nature

Stephen Wasira: ‘No Reforms no Election’ ni Wito wa Fujo na Uvunjaji wa Katiba

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, amesema kauli ya “No Reforms No Election” inayopigiwa chapuo na baadhi ya vyama vya upinzani si hoja ya kisiasa, bali ni wito wa makusudi wa kuvuruga amani na kuvunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza katika mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika wilayani Sengerema Juni 24, 2025, Wasira alisema wito huo unawachochea wananchi hususan vijana, wazee na wanawake, kuacha shughuli zao halali na kushiriki katika vitendo vya fujo kwa lengo la kuzuia uchaguzi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na taratibu za nchi.

“Kuna chama kimoja kinaitwa CHADEMA na kinasema No Reforms No Election — kinawataka vijana, wazee na akina mama eti muungane nacho, mvunje Katiba, mfanye fujo mzuie uchaguzi? Hivi unaweza kuja kuwaambia watu wazima wenye akili timamu mtuunge mkono tuvuruge nchi?”

Wasira alitumia mfano wa wachimbaji wa madini wa Katoro aliokutana nao hivi karibuni, akieleza kuwa ni watu walioko kwenye shughuli halali za kiuchumi, na kuwaeleza wasikubali kupotoshwa.

“Nyinyi mnachimba madini na kila mtu ana shimo lake. Kikinuka, utakimbia na shimo lako? Unakubali mtu akuambie uache shughuli zako halafu uende kupigania jambo ambalo hata hulielewi vizuri?”

Makamu huyo wa Mwenyekiti aliwakumbusha wananchi kuhusu busara ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliyesema kuwa mtu anayekupa hoja ya kipumbavu huku akijua wewe unajua kuwa hiyo hoja ni ya kipumbavu, anakudharau sana.

“Mtu mzima na akili zako unaambiwa uende kupigana. Kupigana kuhusu nini? Uache kulima, kuvua, au kazi nyingine ya kukuingizia kipato halafu uende kwenye fujo usizozielewa?” aliuliza.

Wasira alisisitiza kuwa haki inaweza kudaiwa kwa njia ya amani, lakini si kwa kuvunja haki za wengine au kusababisha vurugu. Alisema ni muhimu wananchi kulinda misingi ya Katiba, kuheshimu sheria, na kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi kama njia ya kistaarabu ya kuleta mabadiliko.

Katika hatua nyingine, Wasira aliwataka Watanzania kutokubali kutumika kama chombo cha vurugu, bali washikamane katika kulinda amani na utulivu wa taifa.

“Kama haki ni yako, unaidai. Lakini hakikisha haki za watu wengine zinalindwa,” alihitimisha.

Related Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *