
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu, ametaka Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Tundu Lissu, aachiwe huru bila masharti akisisitiza kuwa yeye si mhaini.
Akizungumza kupitia televisheni ya mtandao ya chama hicho Jumatano Agosti 20, 2025, Sugu amesema kesi inayomkabili Lissu ni matumizi mabaya ya rasilimali na inazidi kuleta taharuki ndani ya Taifa huku ikiichafua taswira ya Tanzania katika vyombo vya habari vya kimataifa.
Aidha, Sugu amesisitiza kuwa wananchi wana haki ya kidemokrasia ya kuwachagua viongozi wanaowataka bila kulazimishwa na mfumo usiozingatia mageuzi ya kweli ya kisiasa. Ameeleza kuwa kitendo cha wananchi wengi kutokujitokeza kupiga kura katika chaguzi zilizopita ni ujumbe tosha wa kupinga mfumo wa sasa wa kisiasa.
Katika wito wake, Sugu ameitaka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuzingatia hali hiyo na kufanya mabadiliko ya sheria kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025. Amesisitiza kuwa uchaguzi ujao lazima uwe wa haki na wenye ushindani wa kweli ili kulinda amani na mshikamano wa kitaifa.
Mbunge huyo wa zamani wa Mbeya Mjini ameendelea kusisitiza kuwa ni wakati sasa wa kufanya uchaguzi wa haki na ulionyooka, huku akishauri Tume Huru ya Uchaguzi kusitisha mchakato wa uchaguzi ulioanza hadi pale mabadiliko ya msingi kwenye mifumo ya uchaguzi yatakapofanyika.

