Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema imepokea na kuzifanyia kazi kwa makini taarifa na matamko yaliyotolewa na nchi na taasisi mbalimbali za kimataifa kuhusu matukio ya Oktoba 29, 2025, huku ikisisitiza umuhimu wa kuruhusu mifumo ya ndani kuendelea kufanya kazi, ikiwemo Tume ya Uchunguzi iliyoanzishwa kuchunguza vurugu za baada ya uchaguzi.
Katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Serikali imesema, licha ya kuthamini mchango wa jumuiya ya kimataifa katika kukuza demokrasia na maendeleo, imeona “kwa wasiwasi” baadhi ya maudhui ya matamko hayo, hasa ikizingatiwa mazungumzo ya wazi yaliyofanyika kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na wanadiplomasia nchini Novemba 28, 2025.
Tanzania imeeleza kuwa Tume ya Uchunguzi ndiyo chombo halali kitakachobainisha ukweli, sababu, idadi ya vifo na mwelekeo wa matukio hayo, na kwamba ripoti yake ndiyo msingi wa majadiliano ya baadaye. Serikali imezitaka nchi na taasisi za kimataifa kuruhusu taratibu za kitaifa kukamilika bila kuchochea maamuzi ya haraka yanayoweza kuathiri utulivu wa taifa.
Taarifa ya Serikali imetolewa saa chache baada ya mataifa 16 yakiwemo Uingereza, Canada, Norway, Uswisi, Ubelgiji, Denmark, Ufini, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Poland, Slovakia, Hispania, Uswidi, pamoja na Ujumbe wa Umoja wa Ulaya kutoa tamko zito lililosema yana “huzuni na wasiwasi mkubwa” juu ya vifo, majeruhi na madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu wakati na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, na kutaka uchunguzi huru, wazi na shirikishi.
Katika tamko lao la pamoja la Desemba 5, 2025, nchi hizo zilitaka mamlaka za Tanzania kukabidhi miili ya waliopoteza maisha kwa familia zao “haraka iwezekanavyo,” kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa, na kuhakikisha wote waliokamatwa wanapata huduma za kisheria na matibabu. Zilitaja kuwepo kwa “taarifa za kuaminika” kutoka mashirika ya kitaifa na kimataifa zinazodai mauaji nje ya utaratibu wa kisheria, kupotea kwa watu, ukamataji kiholela, na ufichaji wa miili.

