Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kupitia kwa Rais wa Baraza hilo na Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi, Mhashamu Wolfgang Pisa limesema kuandamana ni haki ya raia kama njia ya kufikisha ujumbe au malalamiko ikiwa njia ya mazungumzo imeshindikana cha msingi yawe maandamano ya amani.
TEC imesema inasikitisha kuona kuwa Waandamanaji waliojitokeza siku ya uchaguzi wote waliwekwa katika mwamvuli wa uhalifu huku ikisisitiza adhabu ya Mwandamanaji siyo kuuawa.
“Katika tafakari yetu tunafikiri kati ya mengine mengi maandamano yamesababishwa na matukio ya waziwazi ya mauaji, utekaji, kupigwa na kuumizwa kwa raia bila kuwepo na nia thabiti ya kukomesha maovu hayo ambayo ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 14 Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake kwa mujibu wa sheria.”
“Haki hii imethibitishwa kukiukwa na vyombo vya ulinzi na “Wasiojulikana” ambao wanaonekana wana nguvu kuliko vyombo vya dola.
“Maandamano yamesababishwa pia na kukosekana kwa demokrasia ya kweli ya namna ya kuwapata Viongozi, hili limekuwa kilio cha muda mrefu cha Taifa letu na halijawahi kupatiwa ufumbuzi tangu 2016, Chaguzi zinakosa ushindani wa haki, ukweli, uwazi, uhuru na kuaminika.
“Kwa kuchambua maandamamo, Baraza la Maaskofu limeng’amua kuwa hasira ya wananchi imechochewa pia na kukosekana mahali pa Raia kupeleka na kufanyiwa kazi malalamiko ya kukiukwa haki zao za msingi, kwa baadhi ya mihimili inaingiliwa, vifo vilivyotokea vimeonyesha wazi kuwa vyombo vya usalama vimeshindwa kuthibiti maandamano kwa weledi kwani walitumia silaha za moto, hii ni kinyume na taratibu msingi za Baraza la Umoja wa Mataifa katika kutumia nguvu na silaha za moto ya mwaka 1990 ambazo zinashauri kwamba silaha za moto zitumike tu kama hakuna njia mbadala ya kulinda maisha”
“Hata katika vita huwezi kutumia kila aina ya silaha, maandamano si vita lakini zimetumika silaha zinazotumika katika vita, Askari waliua Ndugu zetu wasio na silaha holela na kwa ukatili mkubwa kama wanyama, kitu kinachotufanya tujiulize binadamu mwenye akili timamu anawezaje kufanya vitendo kama hivyo?”

