Trump Afuta Video ya AI Aliyopost Ikimuonesha Obama na Mkewe Kama Nyani

Rais Donald Trump amelazimika kufuta video fupi kwenye mitandao yake ya kijamii iliyowaonesha Rais mstaafu Barack Obama na mkewe Michelle Obama katika sura ya nyani, baada ya kuibuka kwa wimbi kubwa la ukosoaji kutoka kwa wanachama wa vyama vyote viwili (Republicans na Democrats).

Video hiyo, ambayo inaonekana kutengenezwa kwa teknolojia ya Akili Mnemba (AI), iliwaonesha wanandoa hao wa zamani wa Marekani wakicheza wimbo maarufu wa “The Lion Sleeps Tonight”. Kitendo cha kuwafananisha watu mweusi na nyani kimekosolewa vikali kama matumizi ya taswira za kibaguzi zilizopitwa na wakati.

Ukosoaji mkubwa umetoka kwa Seneta wa Republican, Tim Scott, ambaye ni mshirika wa karibu wa Trump na mwanachama pekee mweusi wa chama hicho katika Seneta. Scott alieleza kushtushwa na picha hizo akisema ni mambo ya kibaguzi zaidi kuwahi kuonekana kutoka Ikulu ya Marekani. Maseneta wengine wa Republican kama Roger Wicker na Pete Ricketts pia walimtaka Trump kuomba radhi.

Msemaji wa Ikulu, Karoline Leavitt, awali alijaribu kupoza ukosoaji huo akidai kuwa kipande hicho ni sehemu ya video ndefu inayomwonesha Trump kama “Mfalme wa Mwitu” (The Lion King) na viongozi wengine wa Democrats kama wanyama tofauti (kama vile tembo, nguruwe, na twiga). Hata hivyo, wakosoaji walibaini kuwa ni Obama pekee ndio waliofananishwa na nyani, jambo lenye historia ya ubaguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari ndani ya ndege ya Air Force One jana, Ijumaa Februari 6, 2026, Trump alidai kuwa yeye aliangalia sehemu ya kwanza tu ya video hiyo inayozungumzia madai ya udanganyifu wa kura na kumpa mtumishi wake aiposti bila kuiona sehemu ya mwisho.

Trump amesisitiza kuwa haoni sababu ya kuomba radhi kwa sababu yeye hakufanya makosa, bali ni makosa ya kiufundi ya wasaidizi wake.

Tukio hili limeibua upya mjadala kuhusu maadili katika kampeni za kisiasa na hatari ya teknolojia ya AI kutumika kuchochea chuki na ubaguzi nchini Marekani.

Related Posts