Tume ya Uchaguzi Zambia Yakanusha Kuja Kujifunza Uchaguzi Tanzanoa

Tume ya Uchaguzi ya Zambia (ECZ) imekanusha taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa maofisa wa tume hiyo wapo nchini Tanzania kwa ajili ya “misheni ya siri” ya kujifunza masuala ya uchaguzi kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu

Katika taarifa rasmi iliyotolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Tume hiyo, Brown Kasaro, tarehe 19 Februari, 2026, ECZ imezitaja taarifa hizo kuwa ni za uongo, zenye kupotosha na zinalenga kujenga mashaka yasiyo na lazima miongoni mwa wananchi.

ECZ imefafanua kuwa Kamishna McDonald Chipenzi, ambaye alikuwa akitajwa katika uzushi huo, yupo nchini Zambia na hajafanya safari yoyote kuelekea Tanzania. Aidha, tume hiyo imesisitiza kuwa hakuna ofisa wake yeyote aliyepo Tanzania kwa sasa kwa shughuli yoyote ile, iwe ya siri au ya wazi.

“Tume inapenda kueleza bayana kuwa tuhuma hizi ni uongo mtupu. Kamishna McDonald Chipenzi yupo hapa Zambia na hajasafiri kwenda Tanzania. Aidha, hakuna ofisa wa ECZ aliyepo Tanzania kwa misheni yoyote,” imeeleza taarifa hiyo kutoka Lusaka.

Tume imetoa wito kwa umma na wadau wa uchaguzi nchini Zambia kuzipuuza habari hizo na kuzitambua kama upotoshaji (misinformation) unaolenga kuleta taharuki.

Uchaguzi huu wa Agosti unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, ambapo Rais wa sasa, Hakainde Hichilema anatafuta muhula wa pili kupitia chama chake cha UPND.

Ingawa chama kikuu cha upinzani (PP) kinaonesha ukinzani mkubwa, Hichilema amepata uungwaji mkono wa kushtukiza kutoka kwa baadhi ya vyama vya upinzani (RPP, NNP, na PNUP) ambavyo vimesifu utendaji wake katika kuimarisha uchumi wa Zambia.

Related Posts