Nature

Tuzo ya Clement Mzize Yawaibua Mastaa

CLEMENT Mzize amekuwa mchezaji wa kwanza Mtanzania kubeba tuzo ya Bao Bora la Mwaka, tuzo aliyoitwaa usiku wa juzi katika hafla ya utoaji wa tuzo za Mwaka za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na sasa unaambiwa tuzo hiyo imewaibua mastaa kibao wakitoa misimamo yao.

Straika huyo wa Yanga aliyekuwa kinara wa mabao wa klabu hiyo katika Ligi Kuu ya msimu uliopita akifunga mabao 14, mawili pungufu ya kinara wa ligi hiyo Jean Charles Ahoua wa Simba, alitwaa tuzo hiyo kutokana na bao alilofunga katika Ligi ya Mabingwa Afrika iliyopita.

Mzize aliwabwaga washindani wake wengine wawili waliokuwa wakiwania nao tuzo hiyo ya bao bora na kufanya baadhi ya wachezaji wa Ligi Kuu kukiri imewapa motisha ya kujituma kwa bidii.

Miongoni mwa waliolizungumzia hilo ni kipa wa Mtibwa Sugar, Costantine Malimi aliyesema: “Ni kitu kizuri kuona mchezaji mzawa kupata tuzo kubwa, hilo linatupa moyo namna ambavyo vipaji vyetu vitaonekana kwa ukubwa zaidi, naamini hilo litampa heshima kubwa Mzize.”

Mchezaji mwingine wa Tanzania Prisons, Jeremiah Juma amesema kitendo cha Mzize kupata tuzo hiyo ya Bao Bora la Mwaka la michuano ya CAF ni faraja na inatia moyo kuona wazawa wanaweza wakafanya vitu vikubwa, tofauti na ilivyokuwa inaonekana kwa wageni miaka ya nyuma.

“Nakumbuka tuzo kama hiyo aliwahi kuchukua mchezaji wa zamani wa Simba, Pape Sakho na sasa imekuja kwa mzawa Mzize hilo litawapa moyo wachezaji wengine vijana kujituma ili kuzifikia ndoto zao kubwa,” amesema Jeremiah.

Kwa upande wa mshambuliaji wa Coastal Union ya Tanga, Adam Salamba amesema: “Kitendo cha Mzize kuchukua tuzo hiyo inaongeza thamani ya Tanzania na kuthibitisha kuna vipaji, kwani wakati wa tuzo imeshuhudiwa na mataifa mbalimbali pia inaleta motisha kwa wengine kujituma kwa bidii.”

Mwingine aliyefurahishwa na hilo ni kipa wa Mbeya City, Beno Kakolanya aliyesema: “Japo Mzize anapitia nyakati za majeraha, lakini hiyo inaleta heshima kubwa sana kwake na atakuwa na bei kubwa sokoni, kwani ametazamwa na mataifa mbalimbali.”

Mbali na wachezaji msanii wa Bongo Fleva, Jay Melody amesema: “Kama kuna nyakati na bahati Mzize anatakiwa kuwa milionea ni hizi, kwanza alikuwa anahusishwa kuhitajika na timu kubwa na sasa kapata tuzo inayoendelea kusisitiza ubora wa kiwango chake.”

Mzize kwa sasa yupo nje ya uwanja kutokana na kujiuguza baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti na alifunga bao hilo katika mechi ya makundi dhidi ya TP Mazembe wakati Yanga ikishinda mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Related Posts