Utopolo Unaofanywa na Marefa Unavyoitia Doa Michuano ya AFCON 2025

Baada ya sifa nzuri ambazo zilielekezwa kwa marefa katika Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2023 zilizofanyika Ivory Coast, mambo yalitegemewa yangekuwa mazuri zaidi katika fainali za 2025 zinazoendelea huko Morocco.

Hata hivyo mambo yameonekana kwenda tofauti katika AFCON awamu hii ambapo idadi kubwa ya mechi zilizochezwa zimeambatana na kiwango cha wastani cha uchezeshaji na baadhi ya mechi maamuzi yamekuwa duni.

Na kwa kiasi kikubwa uchezeshaji usioridhisha umeonekana katika mechi za hatua ya mtoano ambazo ni nyeti na zinazotakiwa kuwa na utafsiri mzuri zaidi wa sheria za mpira wa miguu kwa vile timu inayopoteza mchezo inaaga moja kwa moja na haipati fursa ya kujipanga upya kama ilivyo katika hatua ya makundi.

Dalili mbaya zilianza kujionyesha katika mchezo wa hatua ya 16 bora ambao wenyeji Morocco waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania na kusonga katika hatua ya robo fainali.

Refa Boubou Traore kutoka Mali alitoa maamuzi mengi yaliyoonekana kuinufaisha isivyo halali timu ya taifa ya Morocco huku yakiiathiri timu ya taifa ya Tanzania โ€˜Taifa Starsโ€™.

Alikuwa mkali na mwepesi kuonyesha kadi wachezaji wa Taifa Stars hata kwa faulo ambazo zilionekana nyepesi huku akiwa mzito kufanya hivyo kwa zile zilizofanywa na wachezaji wa Morocco na jambo baya zaidi ni refa hiyo kushindwa kuamua mkwaju wa penalti baada ya beki Adam Masina kumsukuma Idd Seleman โ€˜Nadoโ€™ katika eneo la hatari.

Morocco haohao wakaja kunufaika na makosa ya mwamuzi Dahane Beida katika mchezo wa robo fainali dhidi ya Cameroon ambao waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 ambapo Refa huyo kutoka Mauritania aliinyima mkwaju wa penalti Cameroon baada ya Bryan Mbeumo kuangushwa katika eneo la hatari.

Ikumbukwe Dahane ndiye alikuwa Refa aliyesimamia teknolojia ya video ya usaidizi kwa marefa (VAR) katika mechi ambayo Tanzania ilinyimwa penalti ya Nado na haikuonekana akimshauri Refa Boubou Traore kwenda kufanya marejeo ya tukio hilo.

Wakati matukio hayo yakiwa hayajapoa, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limejikuta lawama tena baada ya kutekeleza ombi la muda mfupi la Morocco kumkataa Refa Amin Omar kutoka Misri ambaye alipangwa kuchezesha mechi yao ya robo fainali dhidi ya Cameroon.

Sababu ambayo ilitolewa na Morocco ilikuwa ni dhaifu na ilishangaza kuona kamati ya marefa ya CAF ikikubaliana na ombi lao ambapo ilidai kwamba ina wasiwasi na refa huyo kwa vile anatoka nchi ya Misri ambayo ina uhasama na taifa lao hivyo ina wasiwasi refa huyo hatowatendea haki.

Lakini cha kushangaza CAF ilitupilia mbali ombi la Misri kumkataa refa Jalal Jiyed kutoka Morocco kwa sababu kama zile ambazo ziliwasilishwa na Morocco hadi refa wa mechi yao dhidi ya Cameroon akabadilishwa.

Matukio kama hayo pamoja na namna marefa walivyochezesha mechi zilizoendana nayo, ni mambo yanayochafua taswira ya CAF na tasnia ya uamuzi wa soka barani humu jambo ambalo sio jema kwa bara la Afrika.

AFCON ni mashindano yenye thamani kubwa zaidi barani Afrika na yanakusanya nyota bira zaidi wa soka ambao wanacheza katika klabu mbalimbali za ndani na nje ya bara hili.

Yanapokabiliwa na tuhuma na matukio yasiyoridhisha ya waamuzi, maana yake hadhi ya CAF na mpira wa miguu Afrika inaporomoka na mwisho wa siku inaweza kuwa chanzo cha anguko lake.

Lakini pia mengi yanapohusu manufaa kwa timu ya taifa ya Morocco, inaweza kutengeneza picha na mtazamo mbaya kwamba CAF inatengeneza mazingira ya Morocco kubakisha taji hilo nyumbani kwa vile ni timu mwenyeji.

Hii ni kinyume na kanuni kuu ya haki ambayo ni kutakiwa kutendeka na pia ni lazima ionekane kama imetendeka.

Kulinda taswira yake na ya marefa wake, CAF inapaswa kutoka hadharani na kujitenga dhidi ya tuhuma zote ambazo zinaelekezwa kwake na marefa katika AFCON 2025.

Inapaswa ionyeshe kwamba haihusiki na aina yoyote ya hujuma au mipango ya kuwabeba wenyeji na kulionyesha hili mbele ya umma.

Related Posts