Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mayeka Saimon, ameeleza kusikitishwa na kitendo cha baadhi ya vijana kuonekana wakishangilia baada ya taarifa za kifo cha aliyewahi kuwa Spika wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Kongwa, Job Yustino Ndugai.
Akizungumza leo Agosti 7, 2025, nje ya nyumba ya marehemu Ndugai katika eneo la Njedengwa jijini Dodoma, DC Mayeka amesema baada ya shughuli za kumpumzisha marehemu kukamilika, watawafuata vijana waliohusika ili kuwaelewesha na kuonesha kuwa tabia hiyo ni kinyume na maadili ya kitanzania.
“Baada ya kumpumzisha ndugu yetu, tutakwenda kuongea na vijana wale kuonesha kwamba ule sio ustaarabu wa Kitanzania na ni utamaduni ambao hatujawahi kuuona Tanzania,” amesema DC Mayeka.
Ameongeza kuwa picha mjongeo zilizosambaa mtandaoni zikionesha baadhi ya vijana wakishangilia kifo hicho zimemshtua, akibainisha kuwa si jambo la kawaida kwa jamii ya Kitanzania.
“Hiki kitendo cha baadhi ya wananchi kushangilia ni kiehemu kidogo sana cha kijiji ambacho baadhi ya vijana ndo wamejitokeza kushangilia. Na kwa kweli ni kitu ambacho kimetushangaza. Kwa hali ya kawaida, mila za Kitanzania, hili jambo linamshangaza kila mmoja kwamba imewezekanaje mtu anashangilia kifo,” alisema.
Amesema ni kweli mtu anaweza kuwa na wapinzani au maadui hasa akiwa mwanasiasa, lakini hakutarajia kuona mtu akishangilia kifo cha mwingine.

