
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imeanza mchakato wa kutunga sheria ndogo itakayoweka utaratibu wa kutoza ushuru kwa Wamiliki wa mabwawa ya kuogelea ( swimming pool ) ikiwa ni hatua ya kupanua wigo wa mapato ya ndani na kuimarisha usimamizi wa huduma hiyo.
Hatua hiyo imetangazwa na Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, Songoro Mnyonge katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichojadili taarifa ya utekelezaji wa robo ya pili ya mwaka wa fedha kuanzia Oktoba hadi Desemba 2025.
Akizungumza katika kikao hicho, Mnyonge amesema kwa sasa sheria ipo kimya kuhusu tozo kwa swimming pool za kibiashara, hali inayosababisha Halmashauri kukosa mapato kutoka kwenye eneo hilo licha ya kuwa ni biashara inayokua kwa kasi katika maeneo mbalimbali ya manispaa ya Kinondoni.
“Sheria imekaa kimya kuhusu swimming pool sisi hatuchaji chochote, unajua unampom-charge Mtu kwamba analipia ile swimming pool ambayo anaifanya pale kwake utamtengenezea na masharti ya kuwa na ile swimming pool, anafuata vipi sheria na taratibu, uokoaji pia unakuaje,”.
“Kwahiyo eneo la swimming pool mpaka sasa hivi sisi Kinondoni tulikuwa tupo kimya hatujakiona kama chanzo cha mapato lakini ukienda huko Kunduchi ni biashara kubwa, ukienda huko Mahotelini ni biashara kubwa na Watu wanalipa fedha nyingi lakini Serikali na Halmashauri haina chochote, hivyo chanzo hicho tunataka tukitungie sheria ili kitambulike kwamba chanzo kipo kinaweza kuingiza fedha lakini vilevile watakapokuwa wanakosea tujue tunawabana katika kifungu gani cha sheria”
