Mkuu wa Jeshi la Uganda ametangaza kuwa amri mpya imetolewa kwa Wanajeshi wa nchi hiyo, kumkamata Bobi Wine, Mwanasiasa wa upinzani akiwa hai au amekufa.
Jenerali Muhoozi Kainerugaba, kupitia kwenye Mtandao wa kijamii wa X, alisema kwamba walikuwa wameacha kumtafuta Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine kwa saa 24 kwa amri ya Kamanda Mkuu Rais Yoweri Museveni, ambaye hivi karibuni alichaguliwa tena kwa muhula wa saba kuiongoza nchi hiyo.
Bobi Wine amekuwa mafichoni kabla ya kutangazwa matokeo ya Uchaguzi wa hivi majuzi nchini Uganda.
Wiki iliyopita, Muhoozi alikuwa amempa Bobi Wine saa 48 kujisalimisha kwa Polisi, jambo ambalo alishindwa kufanya na Operesheni za kijeshi za kumtafuta hazijafanikiwa.
Bobi anadai kuwa kulikuwa na njama ya kumdhuru na kwamba alitoroka nyumbani kwake wakati Wanajeshi walipofika Ijumaa, tarehe 16 mwezi huu, siku moja kabla ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.
Rais Yoweri Museveni alishinda uchaguzi uliopita kwa ushindi wa asilimia 71 , huku mpinzani wake Bobi Wine akipata asilimia 24 ya kura.
