Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, ametangaza mabadiliko makubwa ya kimfumo na kimtazamo ndani ya Jeshi la Polisi kwa maelekezo maalum ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akilenga kulibadilisha jeshi hilo kutoka kuwa la matumizi ya nguvu (Police Force) na kuwa la kutoa huduma (Police Service).
Simbachawene amesema mabadiliko hayo yanalenga kurejesha uhusiano uliopotea, akisema inasikitisha kuona wananchi wakishangilia polisi wanapopata matatizo. Amesema mfumo mpya utadhibiti ukamataji wa kutumia nguvu kubwa kwa makosa madogo.
“Tume imependekeza tusiwe na Police Force bali tuwe na Police Service. Nguvu itumike pale tu inapolazimishwa na sheria kulingana na kosa,” amesisitiza Simbachawene, huku akiweka wazi kuwa haya si maamuzi yake binafsi bali ni utekelezaji wa maagizo ya Amiri Jeshi Mkuu.
