Wawili Kuamua Hatma ya Yao Kouassi Kubaki Yanga

Wakati beki wa kulia Yao Kouassi akirejea uwanjani muda mfupi kabla ya kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili Tanzania, uongozi wa Yanga umewapa watu wawili kibarua cha kuamua kama beki huyo aingizwe katika usajili wao au la.

Beki huyo hayupo katika orodha ya nyota 12 wa kigeni wa Yanga ambao walisajiliwa katika dirisha kubwa la usajili kabla ya msimu kuanza lakini linaweza kuingizwa katika dirisha dogo ikiwa mchezaji mmoja wa kigeni atapunguzwa.

Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe amewataja watu hao kuwa ni Kocha Mkuu, Pedro Goncalves na Kocha wa Utimamu wa miili, Chyna Mokaila.

“Kwasi Attohoula Yao tunachosubiri sasa hivi ni ripoti kutoka kwa kocha wa utimamu wa mwili. Mchezaji ambaye ametoka kwenye majeraha ni ngumu mno kumakadiria kwamba akishapona atarudi. Ikituambia kwamba mchezaji huyu amekamilika kwa asilimia mia, mwalimu atakuwa na namna yake ya kumchunguza Yao kuangalia ubora wake umefika wapi.

“Halafu yeye anatugea sisi mapendekezo yake kwamba sasa hivi mnaweza kumuingiza kwenye usajili, nitamtumia. Amefika kwenye kiwango anachohitaji yeye tumuingize kwenye usajili au tumuache aendelee kufanya naye mazoezi au tumtoe kwa mkopo apate muda wa kucheza. Yote yanaweza kutokea hayo,” amesema Kamwe.

Related Posts