
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe.Dorothy Gwajima, ametangaza kumtafuta mtoto ambaye video yake imekuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii akionekana kuchukua nafasi ya mshehereshaji (MC) katika shughuli mbalimbali za watu wazima.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Waziri Gwajima amesema amepokea taarifa na watu wengi kumtag mara nyingi kuhusiana na tukio hilo, huku akieleza kuwa tatizo si kipaji cha kijana huyo, bali ni aina ya maneno anayoyatumia ambayo hayalingani na umri wake mdogo.
“Wengi mnani-tag sana kuhusu huyu mtoto anachoongea huko online akiwa na kundi la watu wazima wengine wazazi kabisa, wakiwemo wanawake. Wengine wanasema tatizo sio kipaji cha kuwa MC, bali maneno makali anayoyatumia ambayo hayalingani na umri wake, na hapo wapo dada zetu wanafurahi kabisa. Huyu bado mdogo sana, hii imezidi sasa. Daah! Mamlaka husika likomeshe hili,” aliandika Gwajima.
Ameongeza kuwa kipaji cha mtoto huyo kingeweza kukuzwa kwa njia sahihi zaidi badala ya kuendelezwa katika mwelekeo usio na afya kwa maadili na ukuaji wake.
Katika wito wake kwa jamii, Waziri Gwajima aliomba wananchi wenye taarifa wamuelekeze kwa kumpa maelezo ya mahali anapoishi mtoto huyo, kuanzia mkoa, wilaya, manispaa, kata, mtaa hadi nyumba anayoishi, pamoja na kutaja shughuli husika aliyokuwa akiendesha.
“Mengine ustawi wa jamii watajua wakifika huko… Ahsanteni sana,” alihitimisha ujumbe wake.

