Waziri Mkuu, Dkt Mwigulu Nchemba ameagiza kufunguliwa kwa Kanisa la Ufufuo na Uzima, huku akielekeza lipewe miezi sita ya uangalizi katika kuzingatia miiko, masharti na sheria za uendeshwaji wake.
Waziri Mwigulu amesema hayo wakati akiongea na Wakazi wa Kimara na Mbezi Luis Jijini Dar es salaam leo November 24,2025 ambapo ameelekeza kurekebishwa kwa sharti linalotaka kufungiwa kwa nyumba ya ibada iwapo atakosea Kiongozi, akisisitiza anayekosea ndiye aadhibiwe bila kuathiri Waumini kufanya ibada.
“Rais Samia ametoa msamaha kwenye Taasisi za kidini ambazo zilikuwa na msukosuko wa hapa na pale, Mh. Waziri wa Mambo ya ndani upo hapa, baada ya hapa fuatilia utaratibu mzuri ziandikie upya Tasisi za kidini, miiko yao, masharti yao ya uandikishwaji yanafikia wapi na zile ambazo zilikuwa na shida shida wape uangalizi wa miesi sita”
“Natambua ilikuwepo hii moja ya ufufuo na uzima kaifungulie wape masharti ya uangalizi wa miesi sita, ziangalie Taasisi za dini kuzikumbusha miiko na masharti ya usajili waliopewa na nendeni mkayaangalie upya masharti, akikosea mmoja utaratibu wa kufunga kote una madhara kwa Wananchi wetu kwasabbau Ibada ni ushirika wa Binadamu na Mungu sio Binadamu na Aksofu wake, Ibada ni mahusiano kati ya Mwanadamu na Mungu wake kakiangalie vizuri hiki kipengele ili akikosea Sheikh usiadhibiwe Msikiti na akikosea Askofu wasinyimwe Waumini wake kufanya ushirika na Mungu wao”
Kanisa la Askofu Gwajima lilifutiwa usajili, June 2, 2025 kwa kile kilichotakwa na Serikali kuwa lilikiuka masharti ya uendeshaji wake, kwa kuhusisha siasa ndani ya Kanisa.

