Katika ulimwengu wa burudani na urembo nchini Tanzania kuna majina ambayo yana alama zisizofutika. Siyo tu kwa mafanikio yaliyoyapata, bali uwezo wa kuziona fursa na kuzitumia.
Miongoni mwa majina hayo ni Wema Isaac Sepetu, anayejulikana zaidi kama Wema Sepetu, mwanamke aliyeijenga safari yake kutoka jukwaa la urembo hadi kuwa mmoja wa waigizaji maarufu na wenye ushawishi mkubwa katika tasnia ya filamu.
Safari yake ya mafanikio ilianza mwaka 2006 aliposhinda taji la Miss Tanzania, ushindi uliomfungulia milango ya kutambulika kitaifa na kimataifa. Hata hivyo, nyuma ya ushindi huo kulikuwa na ndoto, jitihada na uthubutu wa msichana aliyekuwa anaamini katika uwezo wake.
“Nilipoingia Miss Tanzania sikuwa najua maisha yangu yangekuja kubadilika kwa kiwango kile. Nilikuwa na ndoto tu ya kufanya jambo kubwa, lakini sikuwa najua ni kwa namna gani. Ushindi ule ulinipa mwanga mpya wa kuona kuwa ninaweza kufika mbali zaidi,” anasema Wema.
Baada ya ushindi huo, alipata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa ya Miss World, hatua iliyompa uzoefu mkubwa na kumfungulia milango ya fursa mpya katika maisha yake.
“Miss Tanzania ilinifundisha kujiamini, kusimama mbele ya watu na kuamini thamani yangu. Ilikuwa ni hatua muhimu sana katika kunijenga kama mwanamke na kama kiongozi wa baadaye,” anasema.
Baada ya mafanikio katika urembo, Wema aliamua kujaribu kipaji chake katika uigizaji, uamuzi uliogeuka kuwa mwanzo wa safari mpya yenye mafanikio makubwa.
“Nilipoingia katika filamu nilijua ninaanza kitu kipya kabisa. Haikuwa rahisi mwanzoni, lakini nilikuwa tayari kujifunza na kukua. Nilijua kama nitajituma nitaweza kufanikiwa,” anasema.
Miongoni mwa filamu zake za mwanzo ni A Point of No Return, ambapo alipata nafasi ya kufanya kazi na hayati Steven Kanumba, mmoja wa waigizaji waliokuwa na ushawishi mkubwa katika tasnia ya filamu nchini.
“Kufanya kazi na Kanumba kulinifunza mambo mengi sana. Nilijifunza nidhamu ya kazi, kujituma na umuhimu wa kuichukulia sanaa kwa uzito. Ilikuwa ni shule kubwa kwangu,” anasema.
Tangu wakati huo Wema ameonekana katika filamu nyingi na kujenga jina lake kama mmoja wa waigizaji wenye mafanikio makubwa. Umaarufu wake uliendelea kukua na kuwa miongoni mwa sura zinazotambulika zaidi katika tasnia ya burudani.
Filamu zingine za kukumbukwa ni pamoja na House Boy, Crazy Tenant, Dj Ben, Basilisa, The Diary, Lerato, 14 Days, Tafrani, White Maria, Sakata, Red Valentine na Family Tears.
KUJENGA NDOTO BINAFSI
Mbali na uigizaji, Wema aliamua kupanua wigo wake kwa kuanzisha kampuni yake ya uzalishaji wa filamu, Endless Fame Productions, hatua aliyosema ilikuwa sehemu ya kutimiza ndoto yake ya kuwa zaidi ya muigizaji.
“Nilianzisha Endless Fame Production kwa sababu nilitaka kuwa sehemu ya maamuzi, siyo tu kuwa mbele ya kamera. Nilikuwa na ndoto ya kuzalisha kazi zangu mwenyewe na kusaidia kukuza tasnia ya filamu,” anasema.
Pia alijaribu kuingia katika upande wa muziki kupitia Endless Fame Label, akionyesha dhamira yake ya kupanua mchango wake katika sanaa. Ingawa safari hiyo haikukosa changamoto, anaamini kila hatua aliyopitia ilikuwa sehemu ya kujifunza.
“Si kila kitu kinakwenda kama unavyopanga, lakini kila changamoto inakufundisha kitu. Nimejifunza kuwa mafanikio yanahitaji uvumilivu na kuendelea kupambana hata unapokutana na vikwazo,” anasema.
CHANGAMOTO NA KUSIMAMA UPYA
Kama ilivyo kwa wasanii wengi wenye mafanikio, safari ya Wema haikukosa changamoto. Anakiri kuwa kulikuwa na nyakati ngumu, lakini hakuruhusu changamoto hizo zimzuie kuendelea mbele.
“Maisha yana changamoto zake, lakini nilijifunza kuwa muhimu ni jinsi unavyoamua kukabiliana nazo. Nilichagua kusimama, kujifunza na kuendelea mbele,” anasema.
Anaongeza kuwa changamoto hizo zimemjenga kuwa mwanamke mwenye nguvu zaidi na mwenye uwezo wa kukabiliana na mazingira yoyote.
“Kila changamoto imenifanya kuwa mtu bora zaidi. Leo ninaelewa thamani ya uvumilivu, kujituma na kujiamini,” anasema mrembo huyo.
UJUMBE KWA WANAWAKE
Kupitia safari yake, Wema anaamini kuwa wanawake wana uwezo mkubwa wa kufanikiwa ikiwa watajiamini na kusimamia ndoto zao.
“Mwanamke, usiogope kuota ndoto kubwa. Usiruhusu mtu yeyote akuambie huwezi. Kama unaamini katika ndoto yako na uko tayari kufanya kazi kwa bidii, utafanikiwa,” anasema.
Anaongeza kuwa mafanikio ya kweli hayaji kwa urahisi, bali kwa kujituma na kuwa na msimamo kuyatafuta.
“Mafanikio yanahitaji kujitoa, kujifunza na kutokata tamaa. Kikubwa ni kuendelea mbele hata wakati mambo ni magumu,” anasema.
MAFANIKIO, MSUKUMO KWA WENGINE
Leo hii, Wema Sepetu si tu mshindi wa taji la urembo au muigizaji, bali ni alama ya uthubutu na mafanikio kwa wanawake wengi. Ameonyesha kuwa mwanamke anaweza kuanza na ndoto ndogo na kuijenga hadi kuwa mafanikio makubwa.
Safari yake kutoka katika jukwaa la Miss Tanzania hadi kuwa mmoja wa waigizaji wenye ushawishi mkubwa ni ushahidi kwamba kwa kujiamini, kujituma na kuwa na malengo, mwanamke anaweza kufikia mafanikio makubwa.
Hii inaonyesha pia kuwa Wema ni mwanamke aliyethubutu kuota ndoto, akapambana kuzitimiza na kuendelea kuwa chanzo cha matumaini kwa wanawake wengi wanaotamani kufanikiwa katika maisha yao, hasa katika urembo
