Baada ya kuchezwa michezo minne ya hatua ya makundi katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Kundi B linaendelea kuwa na ushindani mkubwa huku timu tatu zikiwa bado kwenye mbio za kufuzu hatua ya robo fainali.
Nafasi ya kwanza inashikiliwa na Al Ahly SC ya Misri, mabingwa watetezi wa michuano hiyo, wakiwa na pointi 8 baada ya kucheza michezo 4. Al Ahly wanaongoza kundi hilo wakiwa na tofauti nzuri ya mabao +5, hali inayowaweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu mapema.
Young Africans SC (Yanga) ya Tanzania inashika nafasi ya pili kwa pointi 5, sawa na AS FAR ya Morocco, lakini ikipanda juu kutokana na kigezo cha Head to Head. Licha ya Yanga kuwa na tofauti ya mabao -1, ushindi wao wa bao 1-0 dhidi ya AS FAR Rabat katika mchezo wa kwanza wa kundi uliochezwa Zanzibar, bao pekee likifungwa na Prince Dube, umeipa Yanga faida katika upangaji wa msimamo wa kundi hilo.
Kwa mujibu wa kanuni za CAF, timu zinapokuwa na pointi sawa, huangaliwa kwanza matokeo ya mechi za ana kwa ana (Head to Head) kabla ya tofauti ya mabao ya jumla, jambo lililoifanya Yanga kushika nafasi ya pili.
AS FAR Rabat wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 5 na tofauti ya mabao 0, huku JS Kabylie ya Algeria ikishika mkia wa kundi kwa pointi 2 na tofauti ya mabao -4.
Katika mchezo ujao wa Kundi B, Yanga itakuwa ugenini dhidi ya AS FAR Rabat, mchezo unaotarajiwa kuwa wa ushindani mkubwa na wenye umuhimu mkubwa katika hatma ya kufuzu kwa timu zote mbili.
