
Kiongozi Mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema Jimbo la Kinondoni lina nafasi kubwa ya kuleta mageuzi ya kimaendeleo endapo litaongozwa na Kiongozi mwenye maono ya kweli, na kudai kuwa kwa sasa maeneo mengi yameuzwa ikiwemo Viwanja vya Biafra na ameahidi ACT ikishinda watarudisha maeneo hayo kwa Wananchi.
Zitto amesema hayo wakati akimnadi Mgombea Ubunge wa Kinondoni kupitia Chana hicho Rahma Mwita katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi ndani ya Kata ya Tandale, Jimbo la Kinondoni Jijini Dar es salaam leo Septemba 29, ambapo amesema umasikini unaowakabili Wakazi wa Kinondoni unaweza kupunguzwa endapo Viongozi wataweka maslahi ya Wananchi mbele.
“Tusikubali hili kuchagua Wabunge na Madiwani wa CCM hawaleti maendeleo ya kweli, hivi sasa tusipokuwa makini kila eneo la wazi linalotakiwa kwa shughuli za Wananchi linaendelea kuuzwa, tusikubali hili tuchague ACT Wazalendo”
Kwa upande wake, Mgombea Ubunge wa ACT Wazalendo katika Jimbo hilo, Rahma Mwita, amewataka Wananchi kumpa ridhaa ili kutekeleza vipaumbele vyake vinavyolenga kuboresha huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha michango isiyo na tija shuleni inafutwa, idadi ya Walimu inaongezwa, shule mpya zinajengwa na huduma za afya zinaboreshwa kwa mfumo wa bima na huduma musingi kutolewa bure.

