Zuchu Anavyomuwinda Tyla Katika Anga za Muziki

Dar es Salaam. Kwa sasa Zuchu ni kati ya wanamuziki wenye nguvu kubwa ya ushawishi Afrika Mashariki kutokana na mafanikio makubwa ya nyimbo zake mahiri kuhusu mapenzi, starehe na maisha.
Anaiwakilisha vizuri lebo inayomsimamia ya WCB Wasafi ambayo kwa miaka zaidi ya 10 sasa imekuwa ikitengeneza mastaa wenye majina makubwa katika muziki kama yeye. Fahamu zaidi.

  1. Zuchu, mwanzilishi wa Good People Gang (GPG), ndiye mwanamuziki wa kwanza wa kike Afrika Mashariki kwa kazi zake kutazamwa YouTube zaidi ya mara bilioni moja, akiweka rekodi hiyo miaka sita tangu ametoka.
  2. Baada ya Diamond Platnumz, D Voice ndiye msanii aliyeshirikiana na Zuchu mara nyingi zaidi, wawili hao wametoa nyimbo sita, na zote kwa asilimia kubwa zimefanya vizuri. Nyimbo hizo ni Nimezama (2023) na BamBam (2023) kutoka katika albamu ya D Voice, Swahili Kid, nyingine ni Nani (2024), Hujanizidi (2024), Baby Mpya (2025) na Baridi (2026).
  3. Zuchu ndiye msanii pekee wa kike wa kwanza Tanzania na Afrika Mashariki, mwenye rekodi ya kuwa na wimbo ambao video yake imetazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 100. Ni kupitia wimbo wake wenye mahadhi ya Afro Pop, Sukari (2021) ambao ulitayarishwa na Trone na Laizer Classic, huku video yake ikiongozwa na Director Kenny.
  4. Video ya Sukari (2021) ilipotoka ilipokewa vizuri ikitazamwa mara milioni moja YouTube ndani ya saa 22 na kumfanya Zuchu kuandika rekodi kama msanii wa kwanza wa kike Afrika Mashariki kufanya hivyo. Na hadi sasa video hiyo imetazamwa zaidi ya mara milioni 118.1, na kupokea maoni (comments) 22,000 ambayo yanaijadili huku mengi yakimpongeza Zuchu kwa kazi nzuri yenye ubunifu.
  5. Zuchu ndiye mwanamuziki wa kwanza wa kike Tanzania kuchaguliwa kuwania tuzo za MTV Europe Music Awards (EMAs) ambazo hutolewa kila mwaka Ulaya. Aliwania kipengele cha Msanii Bora Afrika 2021 akishindana na Ayra Star (Nigeria), Black Sherif (Ghana), Tems (Nigeria) Musa Keys (Afrika Kusini) na Burna Boy (Nigeria) aliyeibuka mshindi.
  6. Zuchu ni mwanamuziki namba mbili Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kuwa na wafuasi (subscribers) wengi YouTube akiwa nao milioni 4.5 tangu ajiunge na mtandao huo Januari 2019.
  7. Aliyemtangulia Zuchu kwa wafuasi wengi YouTube, ni mshindi mara mbili wa tuzo za Grammy kutoka Afrika Kusini, Tyla ambaye ana milioni 5.6 tangu ajiunge na jukwaa hilo mnano Januari 2021.
  8. Baada ya kuachia albamu ya kwanza, Peace and Money (2024), Zuchu alikaa kimya kimuziki kwa miezi sita ndipo akaibuka na wimbo wake, Amanda (2025) uliotayarishwa na S2kizzy.
  9. Albamu hiyo ilishirikisha wasanii kadhaa wa kimataifa akiwemo mkali wa Afrobeats, Yemi Alade kutokea Nigeria ambaye kipaji chake kiliibuliwa na shindano la uimbaji la Peak Talent Show 2009. Hata hivyo, Harmonize ndiye staa wa Bongofleva aliyefanya kazi nyingi na Yemi Alade, mmoja wapo ni Show Me What You Got (2019) kutoka katika EP yake, Afro Bongo.
  10. Umaarufu wa Zuchu ulikuja kupitia Extended Playlist (EP) yake, I Am Zuchu (2020) iliyofanya vizuri hadi kumuwezesha kushinda tuzo ya African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) kama Msanii Bora Chupukizi.

Related Posts