Waathirika wa Maandamano 29 October 2025 Kupatiwa Matibabu ya Kisaikolojia na Tume

Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, imetangaza mpango maalum wa kuwapatia waathirika wote wa vurugu hizo huduma ya kisaikolojia. Hayo yamesemwa jana wakati tume hiyo ikiendelea kuchunguza

Hatua hiyo imekuja kufuatia mashuhuda na waathirika wengi waliojitokeza kutoa ushahidi wao kuonekana kuwa na makovu mazito ya kihisia na msongo wa mawazo uliokithiri.

Mwenyekiti wa Tume hiyo amebainisha kuwa, wakati uchunguzi wa kisheria na utafutaji wa haki ukiendelea, ni jukumu la Tume kuhakikisha kuwa hali ya kiakili ya waathirika inaimarishwa.

Alieleza kuwa madhila yaliyowapata wananchi hao ni makubwa na yanahitaji uingiliaji wa kitaalamu ili kuwasaidia kurejea katika hali zao za kawaida na kuendelea na ujenzi wa taifa.

Katika vikao vya kusikiliza ushahidi vilivyoanza hivi karibuni, Tume imepokea simulizi za kusikitisha kutoka kwa waathiriwa waliofika mbele yake.

Miongoni mwao ni watu waliojeruhiwa kwa risasi, ambapo baadhi yao bado wana vipande vya risasi mwilini mwao. Aidha, wapo waliopata ulemavu wa kudumu kutokana na mashambulizi ya silaha mbalimbali, hali inayowafanya washindwe kumudu maisha yao kama zamani.

“Tumeshuhudia watu wakilia kwa uchungu hapa mbele yetu. Majeraha ya miili yanaonekana, lakini majeraha ya moyoni ni makubwa zaidi,” alisema mmoja wa makamishna wa Tume hiyo.

Aliongeza kuwa kuwakutanisha waathirika hawa na wataalamu wa saikolojia kutaweka mazingira salama ya wao kueleza yaliyomsibu bila hofu wala shinikizo.

Huduma hiyo itahusisha wataalamu waliobobea katika masuala ya “Trauma Healing” (Uponyaji wa Majeraha ya Kihisia). Lengo ni kuwasaidia waathirika kukabiliana na hofu, wasiwasi, na chuki ambazo zinaweza kuwa zimepandikizwa kutokana na vurugu hizo za kisiasa.

Tume inaamini kuwa amani ya kweli haiwezi kupatikana ikiwa waathirika bado wanaishi na maumivu ya ndani yasiyotibiwa.

Tume imetoa wito kwa waathirika wote ambao bado hawajajitokeza kufanya hivyo, ikihakikisha kuwa usalama wao umeimarishwa na kwamba huduma hizi za afya ya akili zitatolewa bila malipo yoyote.

Hatua hii inatajwa kuwa ni sehemu ya mchakato mpana wa maridhiano na kuponya makovu yaliyoachwa na mchakato wa uchaguzi wa mwaka 2025, ili kuliacha taifa likiwa na mshikamano zaidi.

Related Posts